The House of Favourite Newspapers

Ntibazonkiza ‘Saido’ Apitishwa Simba Kutoka Geita Gold Msemaji wa Simba Afunguka

0
Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.

MTAALAMU wa mipira iliyokufa ndani ya kikosi cha Geita Gold, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, amekubalika ndani ya kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Juma Mgunda.

Saido raia wa Burundi, amekuwa akitajwa kuwa kwenye hesabu za kutua Simba ambao wanahitaji huduma yake kwenye dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 16, mwaka huu ili kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo mshambuliaji.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amebainisha kwamba, uwezo wa nyota huyo upo wazi na hakuna ambaye hatambui.

“Saido ni mchezaji mzuri na ana uwezo kwenye kupiga mipira iliyokufa, anaweza kutengeneza nafasi za mabao pamoja na kufunga, hapo unaona namna alivyo bora.

“Tunaheshimu uwezo wake na tunajua kwamba kwa sasa yupo ndani ya Geita Gold akiendelea kutumikia majukumu yake, kama tukimpata basi tutakuwa tumelamba dume,” alisema Ally.

SIMBA WAITWA MEZANI

Katika hatua nyingine, Mkurungezi wa Geita Gold FC, Zahara Michuzi, amewataka Simba kuwasilisha ofa yao kama kweli wapo tayari kumsajili nyota huyo.

Inaelezwa kwamba, Saido alisaini mkataba wa mwaka mmoja ndani ya kikosi cha Geita Gold FC, mwanzoni mwa msimu huu, baada ya kuachana na Yanga. Hivyo mkataba wake umesalia miezi sita kabla ya kumalizika ambapo sasa yupo huru kufanya mazungumzo na timu yoyote inayomuhitaji.

Akizungumza na Spoti Xtra, mkurugenzi huyo alisema, wao kama klabu hawawezi kumkatalia Saido kwenda kokote, zaidi timu inayomuhitaji ipeleke ofa yao ili wamruhusu.

“Tumesikia hizo habari za Saido kutakiwa na Simba pamoja na klabu zingine, hivyo ombi letu kwa klabu zote ni kuwa yeyote anayemuhitaji aje tuone namna tutakavyoweza kufaidika na uhamisho wake, wasiishie kusema tu huko.

“Saido ni mchezaji muhimu sana kwetu, hatuwezi kubisha, lakini hata akiondoka kuna warithi wake wengi, kuna jumla ya wachezaji wanne kutoka timu yetu ya vijana wamepandishwa, hivyo kuondoka kwake kutawafungulia njia wengine ,” alisema kiongozi huyo.

Msimu huu katika Ligi Kuu Bara, Saido amefunga mabao manne, mawili yakiwa kwa mapigo huru. Alifunga kwa mkwaju wa penalti dhidi ya Mtibwa Sugar na aliwatungua KMC kwa pigo la faulo akiwa nje ya 18, ametoa pasi sita za mabao ndani ya ligi.

STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA NA MUSA MATEJA

Leave A Reply