Nuh: Sijawahi Kumchukia Shilole

“Nipe-leke kwa mganga na mimi nataka wanga…
Maana mapenzi yamenikoroga kinoma…
Anichanje chale mwili mzima…
Nisimkumbe hata jina…
Yule gaidi hasidi wa moyo wangu…
Haya mapenzi basi nimeyavulia shati…
Kupendwa ni ajira na mimi sina vyeti…”
BADO sehemu hii ya mashairi kwenye bonge moja la ngoma inayokwenda kwa jina la Jike Shupa kutoka kwa kijana machachari kwenye ramani ya muziki wa Bongo Fleva, Nuh Mziwanda inawashika mashabiki wake.
Jike Shupa ni kolabo ambayo Nuh Mziwanda alimshirikisha Mfalme wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba au King Kiba.
Jina halisi ni Naftali Mlawa japokuwa wengi wamemzoea kwa jina la Nuh Mziwanda Baby.
Nuh amefanya poa na ngoma nyingine kama Hadithi, Sandakalawe, Anameremeta, Mama Ntilie, Mama Ntilie, Msondo Ngoma, Natapatapa na nyingine kibao.
Kwa sasa ameachia mkwaju mpya unaokwenda kwa jina la Busy Body akiwa na rapa mkali Bongo, Ibrahim Mandingo au Country Wizzy.
IJUMAA SHOWBIZ imepiga stori konki na Nuh Mziwanda ambaye amefunguka mengi; kubwa zaidi ni kuhusiana na uamuzi wake wa kufuta tattoo ya aliyekuwa mpenzi wake wa muda mrefu, Zuwena Mohammed almaarufu Shilole. Unajua sababu ni nini hadi kufanya hivyo? Shuka nayo;
IJUMAA SHOWBIZ: Umekuwa na staili ya kuchelewesha kutoa ngoma labda tatizo liko wapi?
NUH MZIWANDA: Ni kweli, ila kwa sasa sitakuwa nachelewesha kuachia mangoma kama ilivyokuwa awali, nitawapa mashabiki back to back (ngoma baada ya ngoma).
IJUMAA SHOWBIZ: Maana mara ya mwisho kuachia ngoma ulikuwa na rapa Stamini yapata miezi tisa sasa…
NUH MZIWANDA: Ni kweli ila hivi karibuni nina mpango wa kuachia ngoma nyingine na nyingine tena.
IJUMAA SHOWBIZ: Mipango yako iko vipi kwa sasa hasa kuzidi kulikuza jina lako?
NUH MZIWANDA: Kikubwa ni kufanya kazi nzuri ambayo itapendwa na mashabiki, kuwa na heshima kwa kile unachokifanya, NI hilo tu.
IJUMAA SHOWBIZ: Unaonaje ushindani uliopo kwenye muziki kwa sasa ukilinganisha na miaka ya nyuma?
NUH MZIWANDA: Kwa sasa lazima ushindani uwe mkali kwa sababu kila mtu amekuwa mjanja tofauti na awali, ubunifu umekuwa ni mwingi sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Sasa hivi upo kwenye uhusiano wa kimapenzi au?
NUH MZIWANDA: Ndiyo, nipo kwa nini nisiwepo wakati mimi ni mwanaume rijali?
IJUMAA SHOWBIZ: Unaonekana unampenda sana mpenzi wako…
NUH MZIWANDA: Kwa nini nisimpende kwa sababu ndiye mpenzi wangu.
IJUMAA SHOWBIZ: Yeye ndiye amekuambia ufanye hivyo ulivyofanya?
NUH MZIWANDA: Kwani nimefanya nini mbona sikuelewi?
IJUMAA SHOWBIZ: Huelewi nini, kwani umeandika nini mitandaoni?
NUH MZIWANDA: Labda unikumbushe.
IJUMAA SHOWBIZ: Kuna posti umeweka kwamba umeamua kufuta tattoo ya mwanamama Shilole ambayo umedumu nayo yapata miaka mitano ambapo umeandika; “Kwanza mara ya kwanza leo nafuta tattoo ya X wangu (2022) nimekaa nayo sana almost 5 year, ila upendo wangu umechelewa sana kufa. Shout out kwa wote niliowatengenezea mazingira, am done kiroho safi…”
NUH MZIWANDA: Hapana, hawezi kuniambia nifute, nimeamua kufanya hivyo mwenyewe maana nimekaa nayo kwenye mwili wangu kwa miaka sasa.
IJUMAA SHOWBIZ: Mashabiki wanadai kwamba siyo akili yako kufanya hivyo huna nguvu hizo, ni mwanamke amekulazimisha…
NUH MZIWANDA: Hawezi kuniambia nifute ila kama watu wanasema hivyo, acha waongee midomo ni yao.
IJUMAA SHOWBIZ: Naona kama moyo bado unakuuma maana umeandika upendo umechelewa kufa, kivipi?
NUH MZIWANDA: Ni mambo ya kawaida tu hayo.
IJUMAA SHOWBIZ: Au bado unampenda?
NUH MZIWANDA: Mimi sijawahi kumchukia Shilole ila kwa sasa siyo kimapenzi tena, nampenda kama rafiki.
IJUMAA SHOWBIZ: Kama hUmchukii sababu ya wewe kufuta tattoo yake ni nini?
NUH MZIWANDA: Naona nimekaa nayo muda sana kwenye mwili wangu ndiyo sababu.
IJUMAA SHOWBIZ: (shout out kwa wote niliowatengenezea mazingira am done kiroho safi) na hii ina maana gani?
NUH MZIWANDA: Sina maana mbaya jamani, kusema hivyo siyo kwamba naumia roho wala nini, mbona nimeshaamua kitambo tu?
IJUMAA SHOWBIZ: Mbona kama unakuwa na wivu kwa waliopita baada ya wewe?
NUH MZIWANDA: Sina wivu na ndiyo maana nikaandika hivyo.
IJUMAA SHOWBIZ: Unamwambia nini Shilole?
NUH MZIWANDA: Namwambia afanye kazi kwa bidii.
IJUMAA SHOWBIZ: Tuachane na mambo ya mapenzi, tukirudi kwenye muziki, mwaka huu umewandalia nini mashabiki wako?
NUH MZIWAND A: Nimewaandalia mambo mengi ila muda ukifika tutaachia kabisa.
IJUMAA SHOWBIZ: Mipango ya kuachia album imekaa vipi kwa upande wako maana naona wasanii wengi wanafanya hivyo?
NUH MZIWANDA: Ni kitu kizuri sana msanii kuachia album, kinafanya watu waamini kipaji chako. Msanii ukitaka kujua umekamilika kwenye sanaa, lazima utoe album hivyo hata mimi nitatoa.
IJUMAA SHOWBIZ: Wa sanii wengi wamekuwa wakilalamika soko la album linasumbua, kwa upande wako unalizungumziaje?
NUH MZIWANDA: Kutoa album siyo kitu kidogo, unatakiwa kutoa kitu ambacho watu watakubali na siyo kuvurunda hivyo hata mimi nitakuja kulifanya, ila nisiliweke wazi sana.
IJUMAA SHOWBIZ: Je, mipango yako iko vipi kupasua kimataifa zaidi?
NUH MZIWANDA: Ndiyo hivyo tunakomaa, unajua kufikia levo za kimataifa ni jinsi ambavyo wewe unatengeneza muziki wako hadi kufikia levo hizo. Nadhani ni msanii kujiongeza kwa kufanya muziki mzuri, naamini ukifanya hivyo utaona tu mambo yanaenda kwa wepesi.
IJUMAA SHOWBIZ: Unadhani ni kitu gani kinachowakwamisha wasanii kufika mbele zaidi?
NUH MZIWANDA: Naweza kusema wasanii tunaendekeza sana chuki na ubinafsi umekuwa mwingi. Kitu kingine hatupeani madili na roho mbaya zimetawala.
IJUMAA SHOWBIZ: Ahsante sana.
MNUH ZIWANDA: Karibu tena.
Makala: Khadija Bakari, Bongo
 
			
