Odemba Akimbia Ufaransa

Mwanamitindo wa kimataifa ambaye alijipatia jina kubwa ndani na nje ya Bongo kitambo hicho, Miriam Odemba amefanikiwa kukimbia nchini Ufaransa na kukimbilia nchini Switzerland barani Ulaya.

 

Odemba alihamishia makazi yake nchini Ufaransa kutoka Tanzania miaka kadhaa iliyopita, lakini sasa amelazimika kukimbilia Switzerland kujiepusha na janga la kusambaa kwa Virusi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID-19.

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA kwa njia ya simu, Odemba alisema, kila kukicha anaiombea nchi ya Tanzania ili janga hilo lisienee kama ilivyo nchi nyingine.

 

“Kuna wakati ninakosa kabisa usingizi nikiiwazia nchi yangu, naumia mno. Mfano mimi hapa nimekuja nchini Switzerland siyo kwamba napenda, najaribu kulikwepa janga hili kwani linatisha mno jamani, watu wanakufa kila siku, naogopa sana,” alisema Odemba.

Mrembo huyo aliendelea kuzungumza kuwa, hakuna kitu kinachouma kama mtu una pesa ndani ya kununua kila kitu, lakini huwezi kufanya lolote kwa sababu huwezi kutoka, ni kukaa ndani tu muda wote na kama kutoka ni kwa machale sana.

 

“Sasa hivi hakuna mtu anaeelewa chochote zaidi ya kufikiria ugonjwa huu maana kila kitu kimefungwa ambacho ungekifanya kikuingizie pesa, yaani ni ndani mwanzo mwisho na pia hata huhitaji kuangalia televisheni kuna wakati unahisi unachanganyikiwa zaidi,” alisema alisema Odemba ambaye ni mama wa mtoto mmoja aitwaye Iris.

 

Stori: IMELDA MTEMA, Ijumaa


Toa comment