The House of Favourite Newspapers

PATCHO MWAMBA: FM ACADEMIA TUMEIUA

Patcho Mwamba Lukusa

PATCHO Mwamba Lukusa ni miongoni mwa Wakongo walioteka tasnia ya burudani Bongo, akiwa ni muimbaji kutoka Kundi la CP Academia ‘Ngwasuma Full Dose’ ambalo zamani lilikuwa linajulikana kwa jina la FM Academia.

Mbali na kuimba Patcho ni muigizaji tangu enzi za marehemu Steven Kanumba. Jamaa huyu aliwika sana kwenye muvi kibao zikiwemo Love and Power, Deception na Young Billionaire. Lakini baada ya Kanumba kufariki, jamaa hawiki tena kwenye muvi, bila shaka kuna jambo limemfanya azime moto.

Mashabiki wake wanapenda kusikia kutoka kwake nini pengine kinamuangusha. Sasa Risasi Mchanganyiko ndiyo mambo yetu, kukusogezea wasanii ambao una kiu ya kuwasikiliza. Huyu hapa Patcho katika mahojiano maalumu:

Risasi: Patcho umepotea sana kaka hasa kwenye muvi, nini sababu hasa?

Patcho: Kiukweli mimi nipo. Na kwa wanafuatilia muvi nimefanya filamu kadhaa ingawa hazilingani ukubwa na zile ambazo nilikuwa ninafanya na marehemu Steven Kanumba. Ndiyo maana ninaweza kuonekana kwamba nimepotea.

Risasi: Unafikiri kwa nini kazi zako haziwiki kama ambazo ulikuwa unafanya na Kanumba?

Patcho: Unajua Kanumba alikuwa mtafiti sana. Alikuwa ni mtu ambaye mpaka anafanya kazi anakuwa amefanya utafiti wa kutosha. Wanasema mtembea bure ni tofauti na mkaa bure. Alikuwa anakwenda Nigeria, Ghana na sehemu mbalimbali kutazama nini wengine wanafanya na yeye anaboresha kwa hapa nyumbani, hiyo ndiyo tofauti kubwa ya kazi zake na kazi za wasanii wengi wa sasa.

Risasi: Kwa hiyo kikubwa unataka kusema ni utafiti ndiyo umefanya soko la muvi liporomoke?

Patcho: Hiyo ni sababu moja tu. Lakini sababu kubwa ni kwamba waigizaji wengi wa sasa ni wavivu na watu wa kuridhika. Ukifuatilia wengi wamebweteka. Sasa unafikiri kwa hali hiyo tasnia inaweza kupanda kwenda wapi?

Risasi: Kwa hiyo unakubaliana na kauli kwamba Kanumba kaondoka na gemu lake?

Patcho: Ni kweli. Mpaka sasa sijaona kiukweli mbadala wake. Unajua wakati tunafanya naye kazi tulikuwa tukisafiri kwenda nchi za nje huko kama Kongo na Burundi tulikuwa tunapokelewa kama mabalozi na viongozi wa serikali. Ni kwa sababu ya kazi nzuri tuliyokuwa tunafanya. Lakini kwa sasa hivyo vitu hakuna ndiyo maana unaona tasnia ni kama imepwaya.

Risasi: Lakini wewe pia ni muigizaji, vipi ‘future’ yako kwenye tasnia hii?

Patcho: Future yangu ni kubwa kiukweli. Ninajipanga na ninajifunza zaidi siku hadi siku ili niweze kuendelea na siku moja ikiwezekana nizibe pengo la Kanumba.

Risasi: Tukirudi kwenye muziki kwa sasa upande wa dansi kwa baadhi ya bendi mambo siyo mazuri, mnapiga shoo chache halafu kiingilio kinywaji, kwa mwendo huu mtafika kweli?

Patcho: Ni baadhi ya bendi kama ulivyosema. Kwa upande wetu sisi CP mambo ni moto, shoo zinaendelea kila wiki.

Risasi: Kwa nini mmebadilisha jina la bendi kutoka FM Academia mpaka CP Academia?

Patcho: Ni uamuzi tu. Tumeamua kuua jina la FM Academia na kuita hilo la CP.

Risasi: Una nafasi ya kuzungumza lolote kwa mashabiki wako kama unalo?

Patcho: Jumanne (jana) nitatambulisha ujio wangu mpya uitwao Yawee. Mashabiki wasiniache katika hili, wanipe sapoti pia.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.