The House of Favourite Newspapers

Penalti Zampa Milioni Bocco

PENALTI tatu alizopiga na kufunga straika na nahodha wa Simba, John Bocco ndani ya mwezi Machi zimemfanya nyota huyo kuondoka na tuzo ya Mchezaji Bora ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Bocco anakuwa fowadi wa tatu wa Simba kuchukua tuzo hiyo ya mchezaji bora baada ya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kuchukua huko nyuma.

 

Staa huyo mwenye mabao 11 katika Ligi Kuu Bara ameibuka mshindi wa tuzo hizo baada ya kuiongoza Simba kushinda mechi tatu huku akifunga mabao manne. Kati ya hayo matatu alifunga kwa penalti.

 

Bocco alifunga kwa penalti katika mechi dhidi ya Stand United Machi 18 kisha akaweka kambani penalti mbili wakati walipopambana na Mbao FC mkoani Morogoro.

 

Mshambuliaji huyo amewafunika mastaa Donald Ngoma wa Azam FC na Jaffari Kibaya ambao aliingia nao fainali.

Kutokana na kuibuka mshindi, Bocco atajinyakulia kitita cha milioni 1 pamoja na king’amuzi kutoka kwa wadhamini TFF.

 

Pia Kocha wa Simba, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji ameibuka kocha bora wa mwezi baada ya kuiongoza Simba kushinda mechi hizo tatu.

Stori: Na Said Ally, Dar

Comments are closed.