The House of Favourite Newspapers

Zahera: Sasa ndiyo mtaijua Yanga leo dhidi ya Ndanda FC

Kikosi cha timu ya Yanga.

YANGA itakuwa ugenini leo, Alhamisi ikivaana na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara ukiwa ni mchezo wa kumi kukutana kwa timu hizo tangu Ndanda ipande.

 

Mchezo huo, utakuwa moja ya michezo migumu ambayo itakuwa na ushindani mkubwa hasa Yanga ambao wamekuwa hawana historia wala rekodi bora katika uwanja huo.

 

Kocha Mwinyi Zahera atatumia mbinu za ziada kuhakikisha anaondoka na matokeo baada ya kupoteza mchezo wa ligi uliopita dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

 

Yanga kwenye uwanja huo, imeshinda mechi moja pekee ya msimu uliopita wa 2017/18 ambapo ilishinda kwa mabao 2-1 na wenyeji wakishinda mara moja tu msimu ambao walipanda ligi kuu 2014/15.

 

Hata ukiangalia msimu huu timu hizo zilipokutana kwenye mzunguko wa kwanza Yanga ikiwa nyumbani ilishindwa kutamba na kuambulia sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

 

Yanga kwenye uwanja huo wa ugenini imefunga mabao mawili pekee huku na wapinzani wao wakifunga idadi hiyohiyo ya mabao.

Kwa sasa Ndanda imekuwa ikipambana kuhakikisha haishuki daraja kutokana na nafasi ambayo wako kwa sasa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

 

Yanga wao wanaongoza ligi wakiwa na alama 67 wakishinda mechi 21 na sare nne ikiwemo ya Ndanda huku Ndanda yenyewe ipo nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na alama 33 na inapambana kuepuka kushuka daraja.

 

Ndanda kupitia Katibu wao, Seleman Kachele alisema: “Ndanda tunahitaji kushinda hapa nyumbani na kuendeleza rekodi ya ushindi wa mechi tano.”

 

Kocha Mwinyi Zahera anasema: “Kutoka sare katika mchezo wa kwanza tuliocheza Uwanja wa Taifa siyo sababu ya wao kupata sare tena kwa mara ya pili, wafahamu kuwa sisi tumefuata pointi tatu Mtwara,”.

 

“Nafahamu wao watakuwa na jeuri ya kuwa nyumbani kwao, lakini hiyo haitufanyi sisi tuogope na badala yake tutawafunga.

 

“Kwani mechi kadhaa tumecheza za ligi tukiwa ugenini na kufanikiwa kupata ushindi, tena tunafurahia kucheza ugenini kutokana na wachezaji kucheza bila ya presha,” alisema Zahera.

 

Kiungo fundi wa Yanga, Mohammed Issa ‘Banka’ na beki wa kati, Andrew Vicent ‘Dante’ wamepona na leo watakuwa sehemu ya kikosi hicho kitakachowavaa Ndanda FC.

 

“Wachezaji hao ni Banka aliyekuwa anauguza enka na Dante yeye goti ambao wamerejea kikosini, hivyo nafurahia kuona wachezaji waliokuwepo kwenye majeraha wakirejea.

 

“Hivyo, wachezaji hao watakuwepo katika sehemu ya kikosi changu kitakachokitumika katika mchezo huo dhidi ya Ndanda baada ya kuridhishwa na viwango vyao katika mazoezi tuliyofanya hapa Mtwara mara baada ya kufika,” alisema Zahera.

Yanga wanacheza mechi hiyo mkoani Mtwara ambapo Rais John Magufuli yupo kwa ajili ya ziara za kiserikali mkoani humo.

Stori: Martha Mboma na Wilbert Molandi

Comments are closed.