The House of Favourite Newspapers

PENZI LA DIAMOND… KIM NANA AMNYOOSHA LYNN!

KITENDO cha mahasimu wawili ambao ni wauza nyago (sura) kwenye video za wasanii wa Bongo Fleva, Lilian Kessy ‘Kim Nana’ na Irene Godfrey ‘Lynn’ kukutana uso kwa uso kwenye Tamasha la Wasafi Festival mjini Mtwara, wikiendi iliyopita, kimeibua mvurugano, Risasi Mchanganyiko limeinyaka.  

 

Kim na Lynn wanadaiwa kutoiva kwenye chungu kimoja kufuatia vita yao ya penzi la staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliyewaongoza Wasafi kwenye tamasha hilo.

 

Katika ‘tripu’ hiyo ya Mtwara kwenye Viwanja vya Nangwanda Sijaona, Kim anadaiwa kumyoosha vilivyo Lynn na kumaliza jitihada zake za kuwania penzi la jamaa huyo. Kwa mujibu wa watu waliomfuatilia Lynn kwenye safari hiyo, ni wazi mrembo huyo aliyeuza sura kwenye Video ya Kwetu ya msanii Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ wa Wasafi hakuwa na furaha baada ya kubaini uwepo wa Kim. “Kiukweli uwepo wa Kim kwenye safari hii umemmaliza kabisa Lynn kwani hakutarajia kwamba na yeye (Kim) angekuwepo na kwamba yeye ndiye angekuwa upande wa pili wa Diamond.

 

“Kama utakuwa uliwafuatilia walipopanda jukwaani utakuwa uliwashuhudia walivyokuwa wakikatana jicho la ukali. “Lakini Kim anaonekana kuibuka kidedea maana tofauti na Lynn, yeye alionekana mwenye furaha huku akikata nyonga kuashiria hakuwa na stresi kama mwenzake.

 

“Hata wakati wa kurudi Dar, Lynn alipanda gari la wanenguaji na njiani alionekana kabisa hana furaha, tofauti na Kim aliyepanda kwenye gari moja na wanamuziki wa Wasafi na kujitwalia mapozi kama yote hivyo kumaliza kabisa umalkia wa Lynn ndani ya Wasafi,” kilinyetisha chanzo chetu kutoka ndani ya Wasafi. Ili kupata undani wa tukio hilo, Risasi Mchanganyiko lilimvaa Kim na kumpa pongezi zake za kutwaa umalkia wa Wasafi ambapo hakuwa tayari kusema chochote.

Kwa upande wake Lynn alipoulizwa na Risasi Mchanganyiko juu ya sakata hilo na kwamba watu wanasema Kim alimnyoosha kwenye ziara hiyo alisema kwa upande wake hakuna lolote linaloendelea kati yake na Diamond kwa sasa. Alisema Diamond akiamua kumuoa Kim, kwa upande wake yeye hana tatizo na kwamba atakubaliana na hilo na kuwapa baraka zote.

 

Lynn ambaye alionekana kutokuwa sawa na mchangamfu kama kawaida yake alisema kwa sasa yupo tayari kuwa wifi wa Kim. “Unajua kuna kitu watu hawakijui kuhusu mimi na Diamond. Mimi na Diamond hatua uhusiano wowote ule.

“Diamond ni mshkaji wangu sana kwa hiyo hata akimuoa Kim haiwezi kuniuma kwa sababu atakuwa wifi yangu na nimebariki amuoe tu wala sina tatizo lolote,” alisema Lynn. Kwa muda mrefu Kim na Lynn wamekuwa hawaivi chungu kimoja tangu zilipoenea stori kwamba wote ni wapenzi wa Diamond baada ya kuachana na mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.

 

Wakati huohuo, taarifa zilizolifikia Risasi Mchanganyiko zilieleza kwamba, ziara hiyo ya Wasafi Festival itaendelea keshokutwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa kisha Jumapili ijayo katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro

STORI: Musa Mateja na Shamuma Awadhi, Risasi

Comments are closed.