The House of Favourite Newspapers

MSHINDI BSS: NIOKOENI NAKUFA

MAISHA hayatabiriki na Waswahili husema hujafa hujaumbika! Mshindi wa Shindano la Bongo Star Search ‘BSS’ mwaka 2009, Paschal Cassian huwezi amini kwamba licha ya kushinda mamilioni ya fedha katika shindano hilo, leo yuko kitandani akiuguza majeraha aliyoyapata kutokana na ajali ya gari.

 

Uwazi lilipofika Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam, alikolazwa kwa ajili ya matibabu, Cassian alishidwa kujizuia kulia na kusema: Niokoeni Nakufa! Akiwa na Biblia yake mkononi kama mfariji wake huku pembeni yake akiketi mkewe, msanii huyo alionekana yuko kwenye mazito ambayo hawezi kujiokoa bila msaada wa wasamaria wema.

 

CHANZO CHA YOTE NINI?

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mara baada ya kupata ushindi wa BSS mwaka 2009 na kujizolea kitita cha shilingi Mil.25, baadaye Cassian aliokoka na kuanza kufanya kazi ya kuhubiri akiwa kama mwimbaji wa Injili na mchungaji.

 

Anaeleza kuwa wakati akimtumikia bwana kwenye mikoa mbalimbali alipata mwaliko mkoani Kigoma ambako wakati anarudi jijini Dar ndipo alipokutana na mkasa wa ajali ya gari ulioyaingiza maisha yake katika historia mpya.

 

“Tarehe 13 mwezi wa 10 mwaka huu nilikuwa nimetoka Kigoma kuhubiri, ambapo nilikuwa nimefanya ziara mikoa yote ya Tanzania, Kigoma ndiyo ulikuwa mkoa wa mwisho. “Nakumbuka wakati tupo njiani kurudi Dar tukiwa eneo la Manyoni (mkoani Singida), mida ya saa 7 usiku, ambapo ndani ya gari tulikuwa watu wanne pamoja na dereva.

 

“Kutokana na safari nyingi za huduma kiukweli tulikuwa tumechoka hivyo tukawa tumepitiwa na usingizi huku muziki wa Injili ukisikika taratibu kwenye gari, ghafla tulishtuka na kuona gari linayumba. “Kwa kuwa gari ilikuwa kwenye mwendo mkali, dereva alihangaika nalo kulirudisha kwenye hali yake ya kawaida lakini hakuweza kwa sababu tairi lilikuwa limepasuka.

 

“Gari lilipinduka mara tatu na kwenda kupiga kwenye bonde kando ya barabara, mimi nilitupwa kutoka siti ya nyuma niliyokuwa nimekaa hadi kutoka nje ambako nilijikuta nimekaa kama mtu aliyekuwa ameketishwa. “Baada ya hapo sikuwa katika hali ya kawaida, nilipoanza kupata fahamu nikaanza kusikia maumivu kwenye nyonga na mguu wa kulia, kumbe nilikuwa nimevunjika.

AMSHUHUDIA DEREVA AKIKATA ROHO

Wakati akiendelea kujitathimini Cassian anasema alipoangalia pembeni alimuona dereva aliyekuwa akiwaendesha akiwa anakata roho. Hali hiyo ilimtisha na kujikuta haja ndogo ikimbana wakati huo hakuwa anaweza kusimama kutokana na mguu wake kuvunjika.

 

“Nikiwa nimekaa palepale nilifanikiwa kuifungua zipu ili nijisaidie haja ndogo lakini cha kushangaza baada ya kuifungua nilikumbana na damu mkononi mwangu, ambapo hizo damu zilikuwa zinatoka kwenye haja ndogo na kuruka juu.

 

“Yaani zilikuwa zinaruka kama kuku aliyechinjwa, zilitoka kwa muda mrefu hatimaye zikakata. “Baadaye yakaanza kutoka mabonge ya damu, nikajua tayari nimepata matatizo makubwa, tumbo pamoja na kibofu, vikaanza kuuma nikawa najaribu kunyanyuka lakini nashindwa kwa sababu wakati huo hakukuwa na mtu aliyejitokeza kutuokoa, wale wenzangu tuliokuwa nao kwenye gari nao walikuwa na hali mbaya.

 

UOKOAJI WAO ULIKUWAJE?

Anaeleza msanii huyo kuwa baada ya dakika nyingi kupita alijitokeza mwanaume mmoja ambaye hata hivyo hakufika pale kwa lengo la kuwakoa lakini alikwenda kuchukua mali zao kisha kutokomea zake.

 

Aliongeza kuwa mara baada ya mtu huyo kufanya wizi huo, kwa kuibia hadi maiti kisha kuondoa ndipo lilipofika gari ndogo lililokuwa limewachukua akina mama ambao hakujua walikuwa wakitokea wapi. “Baadaye likaja gari likiwa na kinamama, walishuka na kuja mpaka sehemu tuliyopo sisi, wakawabeba wale wenzangu wote lakini mwisho wakaniambia mimi kuwa gari lao limeishiwa nafasi na kwamba ilinipasa nibaki eneo la ajali kusubiri msaada mwingine.

 

“Nilipobaki peke yangu nikawa napaza sauti kuomba msaada, mara gari lingine kubwa likafika, wakashuka watu na kuja kuangalia kilichotokea, mwisho wakapiga simu Polisi ambao walikuja na kunipa msaada wa kunipeleka hospitali ya Manyoni kwa ajili ya kuanza matibabu.

MATIBABU YALISAIDIA?

Katika hali iliyomvunja moyo, Cassian anasema alipofika katika hospitali hiyo hakuna alichopatiwa kama tiba hasa bali ilikuwa ni huduma ya kwanza kwa lengo la kuzuia damu isiendelee kutoka ambapo baadaye alisafirishwa kupelekwa hopitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.

 

Hata hivyo tiba ya Dodoma nayo haikuweza kutatua tatizo lake kwani madaktari walimweleza kuwa kibofu chake cha mkojo kilikuwa kimepata tatizo kubwa na kwamba alihitaji uchunguzi wa kina ambapo alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako anapatiwa matibabu hadi sasa. “Nilipofika Muhimbili, nilikuwa na hali mbaya lakini nashukuru Mungu nilipokelewa vizuri na madaktari walinihudumia vizuri.

 

“Hata hivyo, madaktari waliniambia kuwa natakiwa kufanyiwa kipimo ili kujua kibofu kina tatizo gani lakini nilikaa Muhimbili wiki moja bila kupimwa hicho kipimo.

“Ikabidi mke wangu (Getruda Meshack) ahangaike kutafuta fedha ili kipatikane hicho kipimo, akafanikiwa.

 

“Baada kusomwa kwa kipimo niliona kama daktari hakufurahia sana, sijui ni kwa nini lakini akasema natakiwa nirudi nyumbani, nirudi hospitali baada ya miezi 6. “Majibu hayo kusema kweli ndiyo yaliyonikatisha tamaa. Nirudi nyumbani katika hali hii si nakwenda kufa,” alisema Cassian huku akibubujikwa na machozi.

 

Aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa tabia kwa baadhi ya madaktari kutompa ushirikiano wa kutosha, mmoja wa wauguzi anadaiwa kuwaambia kuwa ‘wasipokuwa na fedha za kuwapatia madaktari hawatatibiwa haraka’ jambo ambalo Uwazi haliamini kama mchezo wa fedha mbele bado unaendelea kufanyika katika hospitali hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa katika siku za hivi karibuni.

Aidha, Uwazi lilimshuhudia mshindi huyo wa BSS akiwa na vifaa vya kuhifadhia haja ndogo huku taarifa zikieleza kuwa, Cassian anajisaidia kwa kutumia mpira.

 

CASSIAN AMLILIA MADAM RITA

“Kwanza kabisa sihitaji kumlaumu kabisa huyu (Madam Rita) kwa sababu najua yupo bize na ni mtu anayetazamwa sana na watu wengi, alishawahi kupigiwa simu na kaka yangu mmoja anaitwa Sifael lakini alimjibu kwamba ametoka yupo nje ya nchi, ila baada ya muda kupita nikawa namuona tena kwenye runinga akifanya usaili.

 

“Kama ananisikia sasa hivi naomba msaada wake, najua ana mambo mengi lakini naomba anisaidie asiniache nife, namtumaini yeye na Watanzania wengine kuwa wanaweza kunitoa katika kifungo hiki cha mateso na kuniweka huru. “Hakuna kitu kinachoniuma kama kupoteza uwezo wa kuhudumia familia yangu, nina mke na watoto wanne na wanasoma. “Kila nikitazama maisha naona giza sijui wanangu na mke wangu wataishi vipi katika maisha haya ya majonzi,” alisema Cassian huku akifarijiwa na mkewe.

 

MKE ANENA

Naye mke wa mshindi huyo wa BSS aliliambia Uwazi kuwa kama familia wako katika kipindi kigumu, cha majaribu, mikasa na mateso ya aina yake na hivyo kuwaomba wasamaria wema wajitokeze kuwasaidia ili wavuke katika kipindi hiki kigumu.

 

“Mimi sina cha kusema, wanawake wenzangu wanaelewa mzigo wa kuuguza mume, naomba walioguswa watusaidie. “Najua Madam Rita kwa umaarufu wake anaweza asitoe fedha lakini akasaidia lau kupata matibabu mazuri ili mume wangu aweze kupona,” alisema mke wa Cassian huku naye akishindwa kujizuia kutokwa na machozi.

 

AOMBEWA MSAADA MITANDAONI

Kwa takriban juma zima habari za kuumwa kwa mshindi huyu wa BSS zimekuwa zikienezwa mitandaoni huku wengi wakiendesha kampeni ya kuhamasisha wasamaria wema wajitokeze kumsaidia ili kuokoa maisha yake. Kwa wanaopenda kutoa michango yao wanatakiwa kuwasiliana na Cassian kupitia namba 0688199370 Au 0672936808.

Comments are closed.