The House of Favourite Newspapers

Peter Msechu Anusurika Kifo

MSANII anayebamba na kava ya Ngoma ya Sitabaki Nilivyo iliyoimbwa na Joel Lwaga, Peter Msechu ameweka wazi kwamba amenusurika kupoteza maisha kisa unene alionao.

Akipiga stori na Mikito Nusunusu, baada ya kuulizwa juu ya kupotea kwake kwenye gemu kwa kupunguza vurugu za kuachia kazi kama ilivyokuwa mwanzo, Msechu alisema yupo ‘busy’ anahudumia kwanza afya yake.

 

“Ni kweli nipo kimya kwa maana kwenye gemu kwa sasa ninanusa nusa tu tofauti na ilivyokuwa zamani. Nafanya hivi kwa sababu sasa ninahudumia afya yangu.

“Unajua nilikuwa nimejiachia sana kiasi kwamba nikawa nimefikisha uzito wa kilo 184 jambo ambalo lilikuwa ni hatari sana kwangu,” anasema Peter Msechu.

 

Anaendelea kwamba baada ya kufikisha uzito huo, kuna baadhi ya kazi alijikuta akiwa hawezi kuzifanya, mara kwa mara mwili wake ukawa mzito, wenye uchovu na mapigo ya moyo yakawa yakimwendea kasi.

“Niliamua kwenda hospitali kwa ajili ya kufanya vipimo. Baada ya kufanyiwa uchunguzi niliambiwa tatizo ni uzito maana nina kilo nyingi pamoja na mafuta ambayo ilikuwa imefika hatua yamezunguka moyo.

 

“Nikaambiwa kwa hali ilivyokuwa inakwenda, muda wowote ningezimika tu ghafla kama nisipochukua jitihada za dhati za kupunguza mafuta,” anasimulia Msechu.

Msechu anaendelea kueleza kwamba baada ya kuambiwa hivyo na kuelekezwa mlo ambao anatakiwa kuutumia pamoja na mazoezi ya kufanya, katika kipindi cha miezi mitano amefanikiwa kukata kilo ishirini na ili abaki salama daktari alimwambia anatakiwa kubakiza kilo angalau 80 tu!

STORI: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.