The House of Favourite Newspapers

Pinda: Mfuko wa Fidia wa WCF Utawalipa Wafanyakazi kwa Zaidi ya Miaka 30 Ijayo

0
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akipokea machapisho ya WCF na nembo ya mfuko kutoka kwa Mkuu wa Idara ya TEHAMA, Stephen Goyayi (kushoto) huku Sarah Reuben akishuhudia.

 

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya kazi kubwa kuhakikisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unaweza kulipa mafao stahiki na endelevu, Waziri Mkuu (Mstaafu) Mhe. Mizengo Pinda amesema.

 

Mhe. Pinda ameyasema hayo wakati alipotembelea banda la WCF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere (Maarufu Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
“Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Mfuko huu ili kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili waajiri hususan wa Sekta Binafsi ambao walilazimika kupoteza muda mwingi wakati wafanyakazi wao walipopatwa madhila yaliyotokana na kazi.” Alisema.

 

Mhe. Pinda ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuchangamkia fursa kwa kujiunga na kuwachangia wafanyakazi wao WCF ili kulinda biashara zao na wafanyakazi wao.Amesema, kuna kazi kubwa ya kuelimisha waajiri na wafanyakazi nchini ili kufahamu kwa ufasaha nini wanaweza kupata kutoka WCF.

 

 

Waziri Mkuu (mstaafu) Mizengo Pinda (kushoto), akisalimiana na Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete walipokutana kwenye banda la WCF kwenye viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam Julai 7, 2022. Wengine wanaoshuhudia ni Afisa Uhusiano Mwandamizi WCF, Bi. Sarah Reuben (wapili kulia) na Mwanasheria Mwandamizi WCF, Bw. Deogratius Ngowi.

 

Amepoungeza Mfuko huo kwa kuweka misingi imara na madhubuti iliyowezesha Shirika la Kazi Duniani ILO kuthibitisha uwezo wa Mfuko huu katika ulipaji wa fidia stahiki na endelevu kwa wanufaika wake kwa zaidi ya miaka 30 ijayo.

 

“Nimefurahishwa na tathmini ya ILO kuhusu uhai wa WCF na ulipaji wa fidia ikiwemo malipo ya pensheni kwa wafanyakazi waliopata ulemavu wa zaidi ya asilimia thelathini (30) na wenza wa wafanyakazi waliofariki kutokana na kazi. Hili ndio lengo haswa la kuanzishwa kwa Mfuko huu na Serikali inajivunia sana kuona matunda ya kuanzishwa kwake” alisisitiza, Mhe. Pinda.

 

Alisema kuwa malipo ya fidia kwa wafanyakazi yanaleta hamasa kwa waajiri wote nchini pamoja na wawekezaji kwani kwa kufanya hivyo, Tanzania inakuwa kituo sahihi cha biashara na uwekezaji.

 

Naye Naibu Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), amewahimiza waajiri wote nchini kuchangia WCF ili wafanyakazi wao wanufaike na huduma zinazotolewa na Mfuko endapo wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

 

“Jitahidini mjiunge na WCF na muione hii kama fursa kwenu na sio mzigo kwa sababu itawapunguzia malalamiko yasiyo ya msingi endapo wafanyakazi watapata ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi,” amesisitiza Mhe. Kikwete.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema WCF itaendelea kufidia wafanyakazi waliopata ulemavu kutokana na kazi pamoja na wategemezi wa wafanyakazi waliofariki kutokana na kazi.

 

Leave A Reply