POLISI AMUUA POLISI MWENZAKE KWA RISASI

Konstebo Kulwa Gilbert enzi za uhai wake.

 

Kifo cha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Konstebo Kulwa Gilbert, aliyepigwa risasi kwa bahati mbaya na mwenzake,  kimezua mshtuko kwa ndugu, jamaa, askari wenzake na majirani aliokuwa akiishi nao nyumbani kwake, Ukonga-Mazizini jijini Dar, Gazeti la Uwazi pekee ndilo lenye mkasa mzima wa tukio hilo.

NI SINZA JIJINI DAR

Tukio hilo la kusikitisha lililotokea Jumanne ya wiki iliyopita, majira ya jioni wakati afande Kulwa na FFU wenzake wakiwa na askari wa kampuni binafsi ya ulinzi wakishusha pesa kwa ajili ya kuziweka kwenye mashine ya ATM ya Benki ya CRDB iliyopo Sinza-Mori pembezoni mwa Kituo cha Mafuta cha Big Bon, jijini Dar.

Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Uwazi kuwa, wakati maafande hao wakiwa kwenye harakati za kushusha pesa hizo karibu na mashine hiyo, kulikuwa na askari wa JWTZ aliyekuwa akitaka kutoa pesa kwenye mashine hiyo hivyo afande Kulwa na wenzake walimuamrisha aondoke haraka eneo hilo kwa sababu za kiusalama.

MASHUHUDA WASIMULIA

Kwa mujibu wa mmoja wa mashuhuda hao, Jimmy Kaishozi, mkazi wa Sinza-Meeda, mwanajeshi huyo, baada ya kupewa amri ya kuondoka haraka eneo hilo, aliona kama amedharauliwa na askari hao hivyo aliwataka wamwambie kistaarabu na siyo kumwamrisha.

Kaishozi alisimulia kuwa, hali hiyo ilizua malumbano kati ya askari hao na mwanajeshi huyo ambapo Kulwa alimfuata jamaa huyo akiwa na bunduki mkononi huku akimuelekezea ambapo mwanajeshi huyo aliikamata na kuelekezea mtutu juu, jambo lililoonekana kuwa alikuwa na utaalam wa masuala ya silaha.

 

Kamanda Mambosasa.

“Kitendo hicho kilizidisha taharuki ambapo askari mwingine wa FFU naye alitoka kwenye gari lililokuwa limebeba pesa na bunduki nyingine na kumlenga mwanajeshi huyo, lakini katika hali iliyoonekana kama bahati mbaya, risasi hizo zilimpata afande Kulwa na nyingine ilimlenga mwanajeshi huyo.

“Hapo mapambano yalizidi kukolea kama sinema ya kivita ambapo askari aliyekuwa akilenga shabaha, alipoona amempiga mwenzake, aliikoki tena bunduki na kumpiga risasi nyingine mwanajeshi huyo ambapo afande Kulwa na mwanajeshi huyo, wote walianguka chini na kuanza kutapatapa huku wakitokwa na damu nyingi.

“Ilichukua muda wakigaragara chini hadi walipofika askari wa Kituo cha Polisi cha Kijitonyama (Mabatini) na kuwachukua, sijui walipelekwa wapi,” alisimulia Kaishozi.

KITUO CHA MABATINI

Hata hivyo, habari kutoka Kituo cha Polisi cha Kijitonyama (Mabatini) ambapo mwandishi wetu alifika, baadhi ya polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo, wakisema kuwa majeruhi walikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo wakiwa njiani afande Kulwa aliaga dunia.

MAKAO MAKUU FFU

Mwandishi wetu pia alikwenda Makao Makuu ya Kikosi cha Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU), Ukonga-Madafu jijini Dar ambapo aliwakuta askari wenzake marehemu ambao walionesha hisia za majonzi wakati wakizungumzia kifo cha mwenzao huyo.

Askari hao hawakuwa tayari kuandikwa majina kwa maelezo kuwa hawaruhusiwi ambapo walimwelekeza mwandishi wetu nyumbani kwa marehemu Ukonga-Mazizini jijini Dar.

NYUMBANI KWA MAREHEMU

Mwanahabari wetu alifika nyumbani kwa marehemu, lakini alikuta chumba chake kimefungwa ambapo mtu aliyekutwa nyumbani hapo alisema kuwa, msiba ulihamishiwa Tazara-Mchicha kwa dada yake aitwae Doto ambaye ndiye pacha wake.

Mwandishi wetu alizungumza na majirani aliowakuta eneo hilo ambao walisema kuwa, kifo hicho kilisababisha mshtuko mkubwa mtaani hapo na kuibua majonzi makubwa.

Kutokana na afande huyo kuishi vizuri na majirani zake, mwandishi wetu aliwakuta wakiendelea kuchangisha pesa za rambirambi huku wakiwa na picha ya marehemu.

ACP Muliro Jumanne Muliro.

UJIJI, KIGOMA KWA MAZISHI

Mwanahabari wetu pia alifika alipoelekezwa ulipokuwa msiba huo, lakini alipofika alikuta tayari mwili wa marehemu ulishasafirishwa kupelekwa kijijini kwao, Ujiji mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.

MWANAJESHI MUHIMBILI

Habari kutoka Muhimbili zilidai kuwa mwanajeshi aliyepata kisanga hicho yeye anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo japokuwa hakuna afisa habari yeyote katika hospitali hiyo aliyekuwa tayari kuzungumzia tukio hilo.

“Ni kweli huyo mwanajeshi yupo, lakini chini ya ulinzi mkali, itakuwa vigumu ninyi kumuona,” alisema mmoja wa askari ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini hospitalini hapo.

KAMANDA MAMBOSASA

Alipoulizwa juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa alisema angempigia mwandishi baadaye.

KAMANDA MULIRO

Mwandishi aliamua kumpigia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Muliro Jumanne Muliro na alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema ni vema kuzungumza na Kamanda wa Kanda Maalum.

“Ndugu yangu si unajua kuwa kuna Kamanda wa Kanda Maalum? Mpigie yeye,” alisema Kamanda Muliro.

Alipoambiwa amepigiwa hajajibu swali ndiyo maana akapigiwa yeye RPC, Muliro alisema atampigia yeye Mambosasa.

Mwandishi alimpigia simu tena Kamanda Mambosasa na kumueleza kuhusiana na tukio hilo ndipo akasema yupo chumba cha daktari na akaahidi kumpigia mwandishi baadaye.

MSEMAJI WA POLISI

Hata hivyo, ili kupata undani wa tukio hilo, pia Uwazi lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, ACP Barnabasi Mwakalukwa na kumuuliza juu ya taarifa za tukio hilo ambapo aliomba atafutwe Kamanda Mambosasa.

“Hilo jambo anayepaswa kulizungumzia ni Kamanda Mambosasa, mtafuteni huyo,” alisema Kamanda Mwakalukwa.

UWAZI LAMRUDIA MAMBOSASA

Uwazi lilimrudia tena Kamanda Mambosasa na kumtaka kulizungumzia tukio hilo ambapo alikiri na kusema kuwa, kulikuwa askari waliofanya tukio hilo walimdhania mwanajeshi huyo kuwa ni jambazi.

Haikujulikana mara moja kama polisi aliyempiga risasi mwenzake pamoja na mwanajeshi huyo kama amekamatwa au la.

KUMRADHI

Jina la Konstebo Justine Mtesigwa, ambalo awali lilitumika kwenye habari hii kwenye gazeti la Uwazi leo  kwamba ndiye aliyeuawa lilikosewa, jina sahihi ya aliyeuawa ni konstebo Kulwa Gilbert. Justine na Kulwa walikuwa ni marafafiki na walikuwa wakifanyakazi pamoja Ukonga. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kwa Justine, ndugu, jamaa, marafiki na wafanayakazi wenzake – Mhariri.

Stori: Richard Bukos, Dar.

Loading...

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment