The House of Favourite Newspapers

Polisi Dar Wahofia Kufa Kwa Kipindupindu

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Kiula Kingu

 

BAADHI ya majirani na polisi wa Kituo cha Polisi cha Mabatini jijini Dar, wameibuka na kudai kuwa kutokana mtaro uliopo kituoni hapo kufumuka na kutoa maji machafu ya chooni yakiambatana na kinyesi, wapo hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.

Maji machafu yakiwa yamejitenga pembeni mwa kituo hcho.

Wakizungumza na Uwazi hivi karibuni, baada ya kutembelea kituo hicho, watu hao wanadai kuwa mtaro huo wa maji machafu uliziba baada ya mvua kubwa kunyesha na kufanya eneo hilo kuwa hatarishi kwa majirani na askari wa kituo hicho.

“Yaani hapa sio hawa polisi tu, hata sisi majirani tupo hatarini kulipukiwa na ugonjwa wa kipindupindu, wakipata maradhi haya polisi kutokana na uchafu huu uliopo hapa kituoni, hata sisi majirani tutapa ugonjwa huo na itakuwa aibu kwa jeshi hili na sisi pia,”anasema jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina Maulidi Saidi.

 

 

Mtaro ukitiriisha maji machafu.

 

Uwazi liliongea na baadhi ya askari polisi wa kituoni hapo ambao hawakupenda majina yao kuandikwa kwa sababu ya maadili kazi yao, walisema wanaomba mamlaka husika kuliona tatizo hilo kwani wanafanya kazi kwa shida kutokana na harufu inayotoka kwenye mtaro huo wa maji machafu uliopo ubavuni mwa kituo hicho, umejaa kinyesi huku sehemu ya kuingilia kituoni hapo kukiwa na dimbwi kubwa la maji machafu yanayotishia afya za askari hao.

 

 

Chemba ikipitisha maji hayo.

 

“Bila shaka wewe mwandishi unashuhudia jinsi kinyesi kinavyomiminika kutoka kwenye chemba, watoto huwa wanachezea kinyesi kitu ambacho ni hatari kwetu, tunaziomba mamlaka husika zitusaidie kuondoa hii kero,” anasema askari mmoja kituoni hapo.

 

 

 

“Harufu hii kali ya kinyesi inaingia mpaka ofisini, hivyo ni hatari kwa sababu hata kwenye kantini ileee (akionyesha kantini yao), maji haya machafu yamefika kama unavyoona,” alisema askari mwingine.

Mkuu wa kituo hicho hakuweza kupatikana ili kujua kama kuna mpango wowote uliofanywa wa kurekebisha chemba na kuzibua mtaro unaotiririsha maji hayo.

 

Gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na maofisa wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam kwa njia ya simu lakini simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa.

Stori: Issa Mnally, Uwazi

Comments are closed.