The House of Favourite Newspapers

Polisi Dar Yakamata Silaha Nzito, Matapeli wa Watalii na Benki – Video

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

KUPATIKANA KWA SILAHA BASTOLA MOJA AINA YA LUGER.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata silaha moja Bastola aina LUGER ambayo haikuwa na risasi ndani yake.

Mnamo tarehe 10 Julai 2018 majira ya 03:30 hrs raia wema walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuwa kuna mtu mmoja anamiliki silaha ambapo ufuatiliaji ulifanyika haraka na ndipo alikamatwa mtuhumiwa huyo huko Temeke Kisuma Bar maarufu kama “SUGAR RAY” akiwa na bastola aina ya Luger iliyotengenezwa Jamuhuri ya CZECH yenye namba usajili A.368021. Jina la mtuhumiwa limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

 

WATUHUMIWA WANNE (4) WA KUGHUSHI HUNDI ZA BENKI WAKAMATWA

Jeshi la Polisi Kanda Maalum DSM mnamo tarehe 24 Juni 2018 huko Kariakoo lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa AMIN KIMARO (55) mkazi wa Manzese na wenzake watatu kwa kosa la wizi wa kughushi hundi za benki mbalimbali jijini na kuziweka kwenye akaunti za washirika wake. 

Katika mahojiano na Jeshi la Polisi watuhumiwa hao walikiri kujihusisha na uhalifu huo na walieleza kuwa wamekuwa wakighushi hundi za benki tofauti tofauti na kisha kuziweka hundi hizo katika akaunti ya benki ili kufanikiwa kuiba fedha walizokusudia.

Sambamba na wahalifu hao Jeshi la Polisi linashikilia gari aina ya Toyota IST namba T 819 DED iliyokuwa ikitumiwa na wahalifu hao, simu za mkononi 8, kadi za simu 6 za mitandao mbalimbali, pamoja na deposit slip ya Tsh 1,973,750 ya hundi ya NMB kwa uchunguzi zaidi.

 

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUTAPELI WATALII

Moja ya majukumu ya Jeshi la Polisi ni kulinda usalama na mali za watalii wanaotembelea nchini. Hili linafanywa makusudi tukizingatia kuwa utalii ni sekta nyeti katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi limefanikiwa kumkamata Bw.Omwailimu Sosthenes Binyakusha anayemiliki kampuni inayoitwa Arise Special Sunrise Safaris ambaye aliwatapeli watalii wawili,mmoja anaishi Marekani na mwingine anaishi India (ni mtu na mama yake).

 

Mtuhumiwa alichukua kiasi cha Dola za Kimarekani 5000 na kushindwa kuwapeleka safari walizokubaliana. Kibaya zaidi mtuhumiwa aliamua kuwatelekeza wageni hao hadi walipohudumiwa na serikali. Hivyo, Jeshi la Polisi linamshikilia kwa uchunguzi zaidi. Jeshi la Polisi linapenda kuwaonya watu wote kufanya biashara hii kwa kufuata sheria.

 

Watuhumiwa sita wa ukwapuaji mikoba kwa kutumia Pikipiki @vishandu wakamatwa

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea na oparesheni maalum ya kupambana na wahalifu wa ukwapuaji kwa kutumia pikipiki@vishandu. Mnamo tarehe 21 Juni, 2018 Polisi walifanikiwa kuwakamata watu sita kwa tuhuma za uporaji mikoba kwa kutumia pikipiki katika maeneo mbalimbali ya jiji la DSM.

Watuhumiwa hao ni; Abuu Salum (22) mkazi wa Manzese, Ivod Fransis (23) mkazi wa Kiluvya, Dankan Deogratias (29) Mkazi wa Kijitonyma na wengine watatu wakiwa na mapanga 3, bisibisi na visu 2 ambavyo hutumika kutishia watu ili kukamilisha uporaji wao.

Aidha katika muendelezo wa Oparesheni hiyo tarehe 26 Juni 2018 lilikamatwa gari aina ya Toyota Mark II lenye namba za usajili T. 955 BEM lililokuwa likitumiwa kukwapua mikoba maeneo mbalimbali ya jiji baada ya kutelekezwa na wahalifu hao.

 

KUKAMATWA KWA MAGARI MATATU NA PIKIPIKI NNE ZA WIZI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa kumi na mbili (12) wa mtandao wa wizi wa magari na pikipiki katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na mikoa jirani.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Mohamed Daimu (34) mkazi wa Tunduru Semeni(Ruvuma), Philemon Chona (34) mkazi wa Tabata, Yusuph Matei (50) mkazi wa Tunduru ujenzi, Jumanne Julius (27) mkazi wa Kawe, Ladslaus Michael (29) mkazi wa Mwenge na wenzao saba.
Aidha katika mahojiano watuhumiwa walikiri kuiba magari hayo na kuwa mara baada ya kuyaiba huyauza katika mikoa mbalimbali nchini.

Magari yaliyokamatwa ni Toyota Noah T.234 CCD na T.729 CEZ, Toyota Mark x T.548 DEJ, Pikipiki MC 330 BYN, MC 210 AYS, MC 822 BMP zote aina ya Boxer na MC 903 BGJ aina ya King Lion.
KUKAMATWA KWA waHALIFU WA UVUNJAJI wa majengo. 

 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kuvunja nyumba/ magodauni na kuiba.

Mnamo tarehe 23 Mei 2018 Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa hao ambao ni; Haruna Yusuph (28) Mkazi wa Makongo, Ally Bakari (53) Mkazi wa Buza, Hawa Juma (32) Mkazi wa Tabata na wengine wawili ambapo waliiba katoni 500 za viatu zenye thamani ya Tsh. 600,000,000/= katika ghala la kampuni ya Bata tarehe 21 Mei 2018 majira ya 5:00 usiku.

Aidha watuhumiwa hao walikamatwa na box saba za viatu, mabegi mawili ya viatu, pamoja na gari aina ya Mitsubishi Canter No. T. 686 BWY ambalo lilitumika kubebea mizigo hiyo, katon 71 za bia, mifuko 18 ya sabuni ya unga na injini 4 za Pikipiki, na mabalo 61 ya nguo za mitumba.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.

 

LIBERATUS SABAS-DCP
KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
11 Julai 2018

Comments are closed.