The House of Favourite Newspapers

Polisi Watumia Mabomu Kumkamata Mwenyekiti Aliyemkataa Mtendaji

2

JESHI la Polisi wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi katika Kijiji cha Mwabasabi Kata ya Nyehunge, lilipotaka kumkamata mwenyekiti wa kijiji hicho, Boniphas Kadinda (Chadema) akituhumiwa kufanya mkutano bila kibali.

Tukio hilo lilitokea jana Jumatatu, Agosti 14 kijijini hapo baada ya polisi kufika katika mkutano huo na kudai ni batili kwasababu hauna kibali hivyo mwenyekiti huyo yupo chini ya ulinzi na kabla hawajamkamata wananchi waliokuwapo walizuia asikamatwe.

 

Baada ya kuona hivyo, polisi waliokuwa na silaha za moto walilazimika kupiga mabomu ya machozi na kuwatawanya wananchi hao kisha kufanikiwa kumkamata.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alithibitisha kukamatwa kwa mwenyekiti huyo akidai amekuwa na tabia ya kuwakataa watendaji wa vijiji wanaokwenda kufanya kazi kijijini hapo akiwatuhumu kuwa walikotoka walikuwa wezi hivyo wasipokewe.

 

Kipole ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, alisema kwasasa mwenyekiti huyo anashikiliwa na polisi katika kituo kidogo cha mji wa Nyehunge.

“Pia alifunga ofisi kinyume na utaratibu, hivyo yupo polisi upelelezi ukikamilika atapekwa mahakamni kufunguliwa mashtaka,” alisema Kipole.

 

Ilivyokuwa

Kabla halijatokea sakata hilo akiwa kikaoni huku umati mkubwa wa wanachi waliohudhuria wakimsikiliza mwenyekiti huyo, alisema ajenda kuu nikujadili suala la Ofisa Mtendaji wa kijiji aliyehamishiwa kijijini hapo, Alphonce Mkumbo kama anafaa kwa kuwa alipotoka anatuhumiwa kula mali za wananchi.

“Sisi wanamwabasabi tunapaswa kuelewa kuwa mtendaji huyu kila mtu anajua alikotoka anatuhumiwa kula mali za wananchi wa Kijiji cha Isaka na leo tunaletewa hapa, tunapaswa kuliangalia suala hili kwa upya,” alisema mwenyekiti huyo.

 

Mmoja wa wanakijiji waliohudhuria mkutano huo, Boniphas Mpanduji aliunga mkono hoja na kuwataka wananchi waliohudhuria katika mkutano huo kumkataa mtendaji huyo kuwa hafai kukiongoza kijiji hicho kutokana na kupungukiwa sifa za uongozi.

Mpanduji alisema wamechoka kuwa shamba la bibi kila mara wanaletewa watendaji wasiofaa.

Wakati hayo yakiendelea, ndipo polisi walifika mkutanao wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi na walipofika waliwaeleza wananchi kuwa mkutano huo ni batili kwa kuwa hauna baraka za vikao vya ndani vya halmashauri ya kijiji na wala wajumbe hawapo hivyo hauwezi kufanyika.

 

Ofisa mtendaji Mkumbo anayetuhumiwa alikanusha tuhuma dhidi yake za kula mali za umma.

“Kinachomsumbua mwenyekiti huyu ni kutaka kufanya kazi za utendaji wakati hana dhamana nazo,” alisema Mkumbo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda alisema anafahamu wazi kuwa katika Kijiji cha Mwabasabi kuna matatizo kati watendaji wanaohamia hapo kuingia mgogoro na mwenyekiti wa kijiji hicho wakidai kuwa mwenyekiti huyo anaingilia mambo ya kiutendaji.

Global TV Kenya: Rais Uhuru Kenyatta Awashukuru Wakenya kwa Kudumisha Amani Baada ya Uchaguzi

2 Comments
  1. […] na Risasi Mchanganyiko, Mwenyekiti wa Mtaa wa Temeke, Bakili Mohamed alikiri kusikia taarifa hizo na kufika kwenye familia ya Muba ambapo […]

  2. […] katika mstari wa mbele kusaidia kupambana na uwindaji haramu na biashara ya pembe za ndovu nchini. Polisi jijini Dar es Salaam wanasema wanachunguza waliotekeleza mauaji hayo, wakati huu ikiwa bado haijafahamika ni kwa nini […]

Leave A Reply