The House of Favourite Newspapers

Polisi Yachunguza Chanzo cha Moto Makerere University

0

POLISI nchini Uganda wanachunguza chanzo cha moto uliokiteketeza Chuo Kikuu maarufu, kikubwa na cha zamani zaidi nchini humo cha Makerere, kilichopo katikati mwa mji mkuu Kampala.

 

Taarifa za awali zinaonyesha kuwa huenda moto huo ulianzia kwenye paa, na baadaye kusambaa kwenye sakafu za majengo ya vitengo vya fedha na rekodi za chuo. Maafisa walikabiliana na moto mkubwa kuanzia takriban saa sita usiku hadi asubuhi Jumapili.

Jengo hilo maarufu lililoungua ambalo linafahamika kama Ivory Tower, lenye kuta nyeupe na madirisha ya bluu, ni moja ya majengo yanayotambulisha chuo hicho maarufu barani Afrika.

Picha katika baadhi ya mitandao ya kijamii ya chuo hicho zinaonyesha sehemu ya nje ya kuta nyeupe za chuo hizo zilizoungua na kugeuka kuwa nyeusi, na baadhi ya madirisha yaliyoungua. Ivory Tower pia lina Ofisi ya Naibu Kansela wa chuo hicho pamoja na ukumbi mkuu wa chuo.

Naibu Kansela, Profesa Barnabas Nawangwe, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter , ameelezea tukio hilo kama asubuhi nyeusi sana na akaongeza kuwa uharibifu uliotokea ni wa kiwango cha kutoaminika.

 

Makerere ni mojawapo ya vyuo vikuu vya hali ya juu zaidi barani Afrika, na ndicho Chuo Kikuu cha zamani zaidi katika Afrika Masharariki, ambapo kilianzishwa mwaka 1922 mara ya kwanza kama shule ya ufundi.

 

Viongozi mbali mbali wa Afrika wamepata elimu ya juu katika Chuo cha Makerere akiwemo muasisi wa Taifa la Tanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwandishi maarufu wa vitabu wa Kenya, Ngugi wa Thiong’o, wasomi na viongozi wa kidini kama vile Askofu Mkuu Mstaafu wa Kiangilikana wa New York, John Sentamu.

 

Leave A Reply