The House of Favourite Newspapers

Pombe Kali za Bei Rahisi Zamkera Mbunge Shigongo Buchosa

0

Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo amekemea matumizi mabaya ya  pombe yanayofanywa na baadhi ya vijana wa jimbo hilo wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Shigongo akiwa jimboni hapo akisikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye mikutano ya hadhara alikutana na baadhi ya vijana wakiwa wamelewa majira ya asubuhi, kitendo ambacho kilimsikitisha kuona nguvu kazi ya vijana inapotea kwa kuendekeza ulevi wa kupindukia.

Shigongo akiwa kwenye Kijiji cha Kasheka Kata ya Bangwe alikutana na vijana wakiwa wamelewa chakari huku vijana hao wakimpongeza kwa kazi nzuri anayoifanya jimboni hapa lakini mbunge huyo hakufurahishwa na namna walivyokuwa katika hali mbaya ya ulevi wa kupindukia.

“Vijana wa jimbo hili wanaharibika kwa kunywa pombe vibaya jambo hili sifurahishwi nalo kwani tunapoteza nguvu kazi ya taifa letu kwa kuachilia vijana wetu kujiingiza katika matumizi ya vilevi hasa pombe zinazouzwa kwa bei ya shilingi 500 na 1000. Hali hii inafanya hata wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutumia vinywaji hivi na wanaenda shule wakiwa wamelewa, hii sio sawa kabisa.

“Serikali licha ya kukusanya kodi kwenye makampuni yanayozalisha pombe hizi lakini ni lazima tufanye marekebisho ya sheria ya vileo ambayo itasaidia kulinda vijana wa taifa hili vinginevyo taifa litaangamia kwa kuwa na vijana ambao hawana uwezo wa kufanya kazi kwa kuendekeza ulevi.

“Nitakapofika bungeni mimi kama mbunge wenu moja ya kazi nitakayoenda kufanya ni kuwasilisha hoja binafsi kuhusu marekebisho ya sharia ya vileo ili tutengeneza taifa lenye vijana shupavu na wenye uwezo wa kufanya kazi na kuleta maendeleo ya taifa letu hatuwezi kuwa na taifa ambalo linasifika kwa kunywa pombe,” alisema.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kasheka wamesema vijana wengi wameathiriwa na pombe za viroba ambazo zinauzwa kati ya Shilingi 500 na 1000 ambazo zimewaathiri vijina wengi waliomaliza kidato cha nne na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao baadhi yao hufika shuleni wakiwa wamelewa na wengine kuishi njiani kwenye vibanda vya kuuzia pombe na wanashindwa kwenda shule.

Wameiomba serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan iangalie jambo hilo kwani vijana  wengi wanapotea kwa kunywa pombe za bei rahisi na mamlaka husika zichukue hatua zaidi ya kuzuia pombe hizo ili kuwanusuru vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Stori: Idd Mumba, Ofisi ya Mbunge Buchosa.

Leave A Reply