The House of Favourite Newspapers

PRETTY KIND; AFUNGUKA KUTOKA KIFUNGONI, AMGUSIA ROMA!

Pretty Kind.

 

JINA lake kwenye vyeti ni Suzan Michael ‘Pretty Kind’. Huyu ni msanii wa muvi, moja ya filamu alizoigiza ni Kilio cha Mnyonge, pia ni msanii wa Bongo Fleva.

Pretty ana wimbo mmoja tu uitwao Vidudu Washa, aliomshirikisha mwanamuziki Gigy Money. Amejizolea umaarufu mitandaoni hasa kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram, kutokana na umbo lake lenye mvuto na kutupia picha akiwa amejiachia kihasarahasara.

 

Kutokana na picha hizo zinazopishana na maadili ambazo amekuwa akiposti, ilisababisha mpaka Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza kumfungia kujihusisha na sanaa kwa kipindi cha miezi sita.

Baada ya kutumikia miezi mitatu kati ya sita, juzikati alifunguliwa kuendelea na kazi zake, kwa onyo kali na kutakiwa kuwa balozi wa wasanii wenzake ambao wanamomonyoa maadili, kuhakikisha wanarudi kwenye mstari.

 

Showbiz Xtra, limempata Pretty ambapo amefunguka mambo mengi aliyopitia wakati akiwa amepigwa pini.

Showbiz Xtra: Hongera sana kwa kufunguliwa Pretty.

Pretty Kind: Asante, kwangu ulikuwa ni muujiza na ninamshukuru Mungu kwa kusikia kilio changu.

Showbiz Xtra: Ilikuwaje kwani, wewe na R.O.M.A, ambaye alikuwa amefungiwa pia mliomba msamaha au nini kilitokea?

Roma Mkatoliki.

 

Pretty Kind: Kwa upande wangu, nilikuwa nimeshaandika barua kadhaa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), za kuomba msamaha lakini sikuwa nimejibiwa. Siku moja kabla ya kufunguliwa nikiwa nimekaa tu nyumbani nilishangaa simu ikiingia na kuambiwa natakiwa na Naibu Waziri Shonza.

Siku ya pili nikaenda na kumkuta R.O.M.A na wasanii wengi, baadaye ndiyo tukazungumza na Waziri Harrison Mwakyembe na naibu waziri ambao waliniambia wamenisamehe na ninaweza kuendelea na kazi zangu.

 

Showbiz Xtra: Baada ya kuambiwa hivyo hali ilikuwaje?

Pretty Kind: Nilifurahi kiukweli maana maisha niliyokuwa ninaishi ni Mungu tu mwenyewe anajua. Watu walikuwa wananinyanyapaa na kunifanyia vitendo vingine vya kunidhalilisha.

Showbiz Xtra: Kwa nini watu walikuwa wanakudhalilisha na kukunyanyapaa?

Pretty Kind: Eti sina maadili. Ilifikia hatua wengine wakawa wananiita mkaa uchi. Kuna sehemu nilienda kuulizia fremu kwa ajili ya kuanzisha biashara wakanitimua kisa kufungiwa na hizo picha za mtandaoni. Jamani, maisha yalikuwa magumu kiukweli na kuna wakati nilikuwa ninakaa ndani mpaka nalia mwenyewe.

 

Showbiz Xtra: Maisha ya kawaida ulikuwa unayaendeshaje, maana huna biashara na ulikuwa hufanyi kazi yoyote ya sanaa?

Pretty Kind: Yalikuwa magumu, nilikuwa nakosa hata shilingi mia moja. Nakunywa mpaka maji ya bomba.

Showbiz Xrta: Lakini si una mpenzi, si alikuwa anakupiga tafu kiaina?

Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza (katikati) akiwa na Roma na Pretty.

 

Pretty Kind: Mh! Baada ya kupata matatizo huyo mpenzi sijui hata alipotelea wapi, sina mpenzi kiukweli nipo mimi kama mimi.

Showbiz Xtra: Unamaanisha Nuh Mziwanda?

Pretty Kind: Huyohuyo.

Showbiz Xtra: Si kuna kipindi ulisema mliachana, nilifikiri una mwingine?

 

Pretty Kind: Tulikuwa hatujapotezeana kabisa. Baada ya majanga ndiyo mambo yalienda kombo zaidi.

Showbiz Xtra: Kutokana na mnyoosho huo wa waziri kuna kitu umejifunza?

Pretty Kind: Nimejifunza mengi sana kiukweli. Tena sana. Siwezi kukaa tena uchiuchi huko mitandaoni. Kwa maana jamii ikiamua kukuadhibu, inakuadhibu kweli kiasi kwamba utaionja chungu ya maisha.

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.