The House of Favourite Newspapers

Q-Chillah Anahitaji Msaada wa Kisaikolojia

0
Mwanamuziki, Abubakari Katwila ‘Q-Chillah’.

NA: Boniphace Ngumije | Amani | MAKALA

Listi ndefu ya wanamuziki waliolifikisha gemu la Muziki wa Bongo Fleva hapa lilipo haikamiliki bila kulitaja jina la Abubakari Katwila ‘Q-Chillah.’

Ukiachana na Dully Sykes, Banana Zorro,TID, Bushoke na wengine wengi wenye heshima katika muziki huu, huyu pia ni mmoja wa vijana waliobarikiwa sauti na kujua namna ya kuitumia kwa kuburudisha na kuelimisha.

Siyo siri jamaa anajua, ndiyo maana kuonyesha ubora wake amedumu kwenye gemu kwa muda mrefu.

Yapata miaka kumi na tano akiogelea kwenye Bongo Fleva. Kwa kinywa chake wakati nikizungumza naye tulipokutana kwenye Shoo ya Bushoke iliyofanyika Jumapili iliyopita kwenye Ukumbi wa Next Door, jijini Dar, Q Chillah anasema amelitumikia gemu kwa maumivu makali, katoa machozi na jasho lakini bado utamu anaostahili kuupata hajaufikia.

Akifafanua jambo alipotembelea Global TV Online.

Q- Chillah ameweka wazi kuwa matokeo ya kufika hapo alipo sasa hayajachangiwa na mtu mwingine. Ni yeye mwenyewe aliyeiharibu kazi ya mikono yake.

Kwamba amefika hapo baada ya kuteleza na kudumbukia kwenye dimwi la matumizi ya madawa ya kulevya maarufu kama ‘unga’. Jambo ambalo analijutia kila mara.

Hata hivyo, nitakuwa wa mwisho kumlaumu juu ya kubwia unga mkali huyu aliyewakosha Watanzania na wapenzi wa burudani kwa ngoma kali zikiwemo Siulinikataa, Tanita, Nipende Nikupende pamoja na Beautiful.

Ujana ni maji ya moto, kama walivyo vijana wengi kuteleza na kudumbukia katika mambo ambayo yanawagharimu kwenye maisha yao, nakubali Chillah aliteleza lakini jambo la kufurahisha ni pale alipojitambua na kufahamu alipokuwa ni ‘kuzimu’. Akaamua kuachana na matumzi ya unga na kurudi tena mahali sahihi.

Kwa mara ya kwanza tangu atangaze kuacha dawa hizo za kulevya, Chillah anakwenda kufanya shoo wikiendi ijayo. Shoo ambayo ameipa jina la Miaka Kumi ya Maumivu.

Hili ni jambo la kumpongeza. Anaonyesha wazi juu ya jitihada zake za kurudi kwenye gemu kwa kila hali. Lakini Chillah anaonekana hapendezwi na hali aliyonayo ndiyo maana ameamua kuwa muwazi ikiwezekana apate msaada kutoka kwa wadau wa muziki, kama si wa pesa hata wa kimawazo.

Niseme tu wazi nimemfahamu Chillah kwa muda mrefu sana, kabla hata sijaanza kazi hii ya uandishi. Chillah ni miongoni mwa vijana watanashati, wastaarabu na wapole kuanzia kwenye mazungumzo yao.

Lakini kwa wanaomjua tangu siku za nyuma, Chillah niliyekutana naye juzi ni watu wawili tofauti. Chillah huyu niliyekutana naye kwa muonekano na mazungumzo yake ya kulaumu na kutoa maneno makali kwa baadhi ya vitu au watu waliosababisha afike hapo alipo anaweza kukufanya utilie shaka juu ya kauli yake ya kupiga chini madawa ya kulevya.

Hata hivyo, naamini kuwa Chillah hatumii ‘unga’ tena.  Pengine ana msongo wa mawazo kwa yale aliyopitia. Ana hasira dhidi ya watu waliomkwamisha na mengine mengi ya kumuumiza.

Ni kweli linaweza kuwa jambo gumu yeye kuyaepuka hayo yote ila kikubwa ninachopenda kumwambia ndugu yangu huyu ni kwamba hapo alipo ni simu ya kumshitua na kumfanya atambue bado Watanzania wanampeda.

Nasema wanampenda kwa sababu juzi kwenye shoo ya Bushoke alipopanda jukwaani na kupiga ‘frestyle’ kidogo alipokea shangwe la kutosha jambo linaloonyesha wazi kuwa watu bado wana mahaba naye. Pia hawataki kumuona akipotea kutokana na madawa ya kulevya lakini pia anatakiwa kujisimamia ikiwa kweli ameamua kumshinda shetani wa unga.

Watu wake wa karibu na Watanzania kwa jumla tuna wajibu wa kumsaidia Chillah. Kwa kila hali hata mawazo tu kuhakikisha anaondokana na msongo wa mawazo.

Ingawa nimesema ninaamini Chillah hatumii unga nampa angalizo kototumia mwamvuli wa kuwaaminisha Watanzania kuwa kaupiga chini ila anautumia kwa kificho. Namkumbusha yale ya msanii mwenzake Rashid Makwiro ‘Chid Benz’.

Wakati ‘media’ zikipiga kelele kuwa anabwia unga yeye aliibuka na kukana mara kadhaa na watu wakamuamini, lakini baadaye hali yake ilikuwa mbaya na kila kitu kikawa wazi. Kama unasema umeacha iwe kweli umeacha. Usiseme kwa kuwaridhisha tu Watanzania maana utakuwa unazidi kujimaliza mwenyewe!

 

Leave A Reply