The House of Favourite Newspapers

Rais DK.Mwinyi Akutana na Uongozi wa Shirika la kimataifa la Christian Blind Mission (CBM)

0

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inajitahidi kuboresha mazingira wezeshi kwa watu wenyeulemavu kwenye sekta zote za jamii zikiwemo Usafiri wa umma, Elimu na Afya kwa kuzingatia na kurahisisha mahitaji yao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema hayo leo  Ikulu, Zanzibar alipozungumza na ujumbe kutoka Shirika la kimataifa la Christian Blind Mission (CBM) waliofika kumtembelea.

Alieleza kufurahishwa kwake na ushirikiano uliopo baina ya Serikali na Shirika hilo kupitia Wizara ya Afya Zanzibar.

Dk. Mwinyi amesema Serikali ikiwa kwenye mchakato wa kutoa huduma za Bima ya afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba, kipaumbele zaidi kimezingatiwa kwa watu wenyeulemavu, Zanzibar.

 

Akizungumzia sera ya watu wenyeulemavu ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza sera hiyo kwa vitendo kwa kuzingatia matakwa na mahitaji ya jamii hiyo hata kwenye majengo yote ya umma inaweka mkazo zaidi kwa mahitaji yao ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo na ofisi za Serikali kufikiwa na watu wajamii zote ikiwemo huduma za ngazi na vyoo kuwa na mazingira rafiki kwa watu wote.

Alisema Serikali kwa kuzingatia mpango mpya wa huduma ya usafiri wa Umma imeadhimia kuboresha huduma hiyo kwa jamii, kwa kuwazingatia watu wenyeulemavu na kuangalia uwezekano wa kuwafikia kwa huduma wezeshi huku akieleza wadau zaidi wanahitajika kuunga mkono kwenye sekta ya afya kwa watu wenyeulemavu.

Aidha, aliiomba taasisi ya CBM, kuangalia uwezekano wa kuungamkono suala la ujenzi wa makaazi kwa ajili ya watu wenyeulemavu, kwani Serikali ina nia ya kuboresha huduma hiyo, pamoja na kuwakaribisha wadau wengine wa maendeleo kuunga mkono huduma hiyo kwa Serikali.

Nesia Satoki Mahenge, Mkurugenzi Mkaazi wa CBM, wanashirikana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo wametoa kiasi cha shilingi bilioni moja kwaajili ya kutekeleza mradi wa matibabu kwa watu wenyeulemavu.

Naye, Mkurugenzi Maendeleo Jumuishi CBM, Dominique Schlupkothen alimueleza Dk. Mwinyi kwamba taasisi hiyo inafanyakazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali, taasisi binafsi pamoja na wadau wengine wa maendeleo, mbali na kujikita kwenye kutoa huduma za afya ya macho pia wamejikita na miradi inayoshughulikia maradhi yasiyopewa kipaumbele duniani yakiwemo mabusha, minyoo na maradhi mengine.

Leave A Reply