The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli Akisikiliza Changamoto za Wachimbaji Wadogo – Video

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini (Femata), John Bina amesema Tanzania hakuna masoko rasmi ya uuzaji wa madini jambo ambalo linachangia kukosekana kwa bei elekezi na kuchangia ukwepaji kodi.

 

Bina ameyasema hayo wakati akitaja changamoto nne ambazo ni mitaji, masoko ya uhakika, uchimbaji na tozo zisizo rafiki zinazoikabili sekta ya madini licha ya kuwapo kwa mafanikio mengi yaliyopatikana katika sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo katika mkutano wa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais Magufuli.

 

Amesema Serikali imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana na hali hiyo huku ikichangia uingizwaji wa fedha zisizo rasmi.

“Fedha inatoka nje inaingia kwa njia zisizo rasmi na inatoka kwa njia isiyo rasmi jambo ambalo linasababisha utoroshaji wa madini,” amesema

Amesema zuio la kusafirisha madini yasiyo chakatwa Serikali inapaswa itoe mwongozo ili kujua yawe yamechakatwa kwa kiwango gani ili yaweze kwenda nje.
“Kuna wale wachimbaji waliokumbwa na suala hili huko nje tuangalie tuone ni namna gani tunaweza kufanya, ni ombi,” amesema

 

Akizungumzia suala la mitaji, Bina amesema ili biashara ya madini iweze kufanyika ni lazima benki zitoe mikopo katika sekta ya madini jambo ambalo halifanyiki kwa sasa kwa sababu wachimbaji hawakopeshwi kutokana na madini wala leseni zao.

 

“Hili jambo haliwezekani kwetu tu lakini sehemu nyingine linafanyika. Tutafute mbinu yoyote tukopeshwe ili tuchimbe na hakuna masoko rasmi nchini na hivyo hakuna bei rasmi jambo ambalo linachangia kukwepa kodi,” amesema.

 

Kuhusu tozo na kodi zisizo rafiki, amesema mchimbaji mdogo analipa asilimia 12.03 huku akiiomba Serikali wachimbaji hao walipe kutokana na mazingira.
“Tunajua unataka kujenga nchi kupitia kodi zetu lakini tunaomba ungetuhurumia ukapunguza kidogo.”
“Kampuni nyingine zinakuja kuchimba bila leseni hivyo tunaomba maeneo yaliyotengwa waweze kupewa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao,” amesema.

Comments are closed.