The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli Atuma Salamu kwa Rais wa China

xi-jinpingRais wa China Rais Xi Jinping.

Dar es Salaam. Rais John Pombe Magufuli, ametuma salamu kwa Rais wa China Rais Xi Jinping na kusisitiza kuwa  Tanzania itaendeleza uhusiano na  ushirikiano wake na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa leo (Jumatatu) na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa, salamu hizo zimetolewa na Rais Magufuli baada ya kutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Ulinzi ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) Jenerali Fan Changlong, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

“Nimefurahishwa na ziara yako hapa nchini kwetu, ujio wako unazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zetu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya Hayati Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Mwenyekiti Mao Tse-tung wa China.

“Naomba unipelekee salamu zangu kwa Rais Xi Jinping na umwambie kuwa pamoja na kuendeleza uhusiano na ushirikiano wetu katika kuimarisha majeshi pia tunatarajia kuona China inakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi zetu za maendeleo kwa kujenga viwanda na kushiriki katika miradi mingine ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard Gauge,”amesema Rais Magufuli.

Comments are closed.