Rais Msumbiji asema watu 1,000 wamefariki kwa kimbunga Idai

 

IDADI ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Idai nchini Msumbiji sasa huenda ikawa ya juu na kufikia watu 1,000 Rais Filipe Nyusi amesema.

 

Nyusi aliyakagua kwa ndege maeneo yalioathirika zaidi jana (Jumatatu0 na kusema aliona miili ikielea juu ya mito.

 

Tayari kuna wasiwasi kuhusu maisha ya zaidi ya watoto 100,000 na watu wazima kufuatia kimbunga hicho huku mito katika maeneo yaliothirika zaidi ikivunja kingo zake, kwa mujibu wa habari kutoka shirika la Save the Children.

 

Mafuriko hayo yamezidishwa na kimbunga Idai ambacho kililikumba eneo la kaskazini mwa Msumbiji mnamo tarehe 15 mwezi huu na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, shule, hospitali na miundombinu.

 

Kwa mujibu wa serikali ya Msumbiji,  takriban watu 600,000 wameathiriwa, huku zaidi ya watu 1,000 wakidaiwa kupotea na 100,000 wakihitaji msaada wa dharura mjini Beira.

 

Kiwango cha janga hilo kinazidi kuongezeka kila dakika na shirika la Save the Children lina wasiwasi mkubwa kuhusu watoto na familia walio katika hatari huku viwango vya mafuriko vikizidi kuongezeka,  anasema Machel Pouw mkuu wa oparesheni ya shirika hilo nchini Msumbiji.

 

Save the Children ni mwanachama wa COSACA wakishirikiana na shirika la OXFAM pamoja na lile la CARE na linafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na serikali na taasisi za usimamizi wa majanga ili kuwasaidia watoto walioathirika

 

Kimbunga hicho kilishuka katika mji wa bandari wa Beira siku ya Alhamisi kikiwa na upepo wenye kasi ya hadi kilomita 177 kwa saa , lakini mashirika ya misaada yalifika katika eneo hilo siku ya Jumapili.

 

Mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa aliambia shirika la habari la Uingereza (BBC) kwamba kila nyumba mjini Beira- ambao ni mji wenye wakazi wapatao nusu milioni imeharibiwa.

Loading...

Toa comment