The House of Favourite Newspapers

Rais Museveni Ateuliwa Kugombea Urais kwa Mara ya Sita

Chama tawala nchini Uganda kimemteua Rais Yoweri Kaguta Museveni kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2021. Hii inamaana ya kuwa, kiongozi huyo mwenye miaka 74, na aliyeingia madarakani kwa mtutu wa bunduki mwaka 1986, atagombea urais kwa muhula wa sita.

 

Chama cha National Resistance Movement (NRM) kimekubali, katika kikao kilichoongozwa na Museveni jana Jumatano kuwa ” (Museveni) aendelee kuongoza harakati na taifa mwaka 2021 na kuendelea ili kuondosha vikwazo vya mabadiliko na maendeleo.”

 

Miaka ya nyuma, Museveni aliwahi kusema kuwa, viongozi “wanaodumu” madarakani ndio chanzo cha matatizo barani Afrika. Hata hivyo, wakati akigombea muhula wa tano wa madaraka mwaka 2016, alisema kuwa huo haukuwa muda muafaka kwake kuondoka madarakani kwani bado alikuwa na kazi ya kufanya.

 

Ugombea wake katika uchaguzi ujao unakuja baada ya kusaini kuwa sheria mswada ambao uliondoa ukomo wa urais wa miaka 75. Hata hivyo, kupitishwa kwa muswada huo bungeni kuligubikwa na vurumai kubwa kutokana na kupingwa na wabunge wa upizani.

 

Mahakama ya Upeo ya Uganda mwezi wa Januari imeanza kusikiliza shauri la kupinga mabadiliko hayo ya sheria. Upinzani dhidi ya mabadiliko hayo ya sheria yamemuibua msanii Bobi Wine kama kinara wa upinzani na mwiba mkali dhidi ya serikali ya Museveni ndani na nje ya bunge la Uganda.

 

Tangazo la Museveni kugombea tena lilitarajiwa kutkana na mabadiliko ya sheria lakini wachambuzi wameshangaa kutolewa miaka miwili kabla ya uchaguzi wenyewe. Wiki hii pia rais Museveni amempandisha cheo mwanawe wa kiume na kufikia cheo cha pili kwa ukubwa zaidi jeshini.

 

Kainerugaba Muhoozi sasa amepanda kutoka kuwa Meja Jenerali na kufikia Luteni Jenerali katika jeshi la Uganda. Japo amekuwa mkuu wa vikosi maalumu vya jeshi la Uganda na sasa anahudumu kama mshauri wa rais wa operesheni maalumu, upandaji wake wa vyeo unaonekana ni wa kasi kubwa.

 

Kasi hiyo ndiyo ambayo wakosoaji wa rais Museveni na wanaharakati wanadai ni kielelezo kuwa kuna mipango unaosukwa wa mtoto huyo wa rais kumrithi baba yake. Hata hivyo, Jenerali Muhoozi amekuwa akikanusha kuwa ana mipango ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa.

Comments are closed.