The House of Favourite Newspapers

Rais Mwinyi Amsubiri Maalim Seif Ikulu – Video

0

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, anasuburi uamuzi wa Maalim Seif Sharif Hamad na chama chake cha ACT – Wazalendo katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar (SUK).

 

 

Akizungumza wakati akitangaza Baraza la Mawaziri leo tarehe 19 Novemba 2020, Rais Mwinyi amesema, tayari amewaandikia barua Chama cha ACT – Wazalendo kuomba jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.

 

 

Amesema, amechukua hatua hiyo kwa kuwa ni takwa la Kikatiba kwamba, chama kinachofikisha ama zaidi ya asilimia 10 ya kura, kinajumuishwa katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

 

 

“Chama cha ACT – Wazalendo kina idadi ya viti vya uwakilishi waliochaguliwa, ndio maana nimeacha nafasi mbili endapo watakuwa tayari.

 

 

“…lakini ukweli ni kwamba, hadi leo hawajaenda kuapishwa, kwa hiyo hawajasajiliwa kwa hiyo lazima tuwape muda wa kikatiba, hiyo ndio sababu,” amesema Rais Mwinyi baada ya kuulizwa na mwandishi kuhusu nafasi mbili alizoacha na mpango wake wa kuhusisha wapinzani kwenye serikali yake.

 

 

 

Katika uchaguzi mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 visiwani Zanzibar, Rais Mwinyi alitangazwa kupata jumla ya kura 380,402 sawa na asilimia 76.27, ambapo Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha ACT – Wazalendo alitangazwa kupata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

 

 

Hata hivyo, Maalim Seif na chama chake waligomea matokeo hayo wakidai kuwepo kwa udanganyifu na kasoro zilizo wazi. Rais Mwinyi amesema, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, mgao wa nafasi za mawaziri kwenye baraza hilo inategemea na uwiano wa idadi ya viti vya wawakilishi wa kuchaguliwa.

 

 

Pia Rais Mwinyi amekumbusha, kwamba wakati wa kampeni zake kusaka urais visiwani humo, alieleza dhamira yake ya kuwaunganisha Wazanzibari na kuwa wamoja.

 

 

“Kama mlivyoshuhudia, wakati wa kampeni nilisema, tunataka Wazanzibari tuwe wamoja. Nilisema, tuko tayari kutekeleza matakwa ya kikatiba yanayotaka chama cha upinzani kinachopata zaidi ya silimia 10, kiweze kushiriki katika serikali,” amesema.

Leave A Reply