The House of Favourite Newspapers

Rais Obama hatimaye ajiunga Facebook

0

Barack Obama

Rais Barack Obama.

RAIS wa Marekani, Barack Obama hatimaye amejiunga na mtandao wa kijamii wa Facebook na kuandika ujumbe wake wa kwanza wa kuhimiza watu kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

obama new

Ikulu ya White House kwenye ukurasa huo imeweka video ya Obama akitembea katika eneo la South Lawn katika ikulu ya White House.

Hatua yake ya kujiunga na Facebook, ambao ni mtandao wa kijamii wenye zaidi ya watumiaji bilioni moja, inaonekana kama juhudi za kiongozi huyo kuwafikia zaidi vijana na makundi mbalimbali ya watu.

“Natumai mtauchukulia huu kuwa ukumbi ambao tunaweza kutumia kujadiliana kuhusu masuala muhimu kuhusu taifa letu,” anasema kwenye video hiyo.

Obama anaonekana akitembea kwenye bustani hiyo ambayo imekuwa chini yake kwa miaka saba iliyopita, ambayo kama anavyosimulia, ina mbweha, mwewe na vichakuro.

Lengo kuu la kisiasa hata hivyo linaonekana kuhimiza ulimwengu kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Obama atazuru Paris mwezi Desemba, kutafuta uungwaji mkono wa mkataba wa kuweka vikwazo kwa mataifa kuhusu viwango vya utoaji wa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani.

Kutokana na hali kwamba Bunge la Congress linadhibitiwa na Chama cha Republican, ambacho hakijatambua hatari inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi, anahitaji kutafuta uungwaji mkono zaidi hata nyumbani.

White House imesema inatumai Facebook itasaidia kama ukumbi wa kubadilishana mawazo.

“Ukurasa huu utawapa Wamarekani jukwaa la kubadilishana mawazo yao na Rais kuhusu masuala ambayo wanayajali sana,” amesema naibu mkurugenzi wa mkakati wa dijitali katika White House, Kori Schulman.
Rais Obama alijiunga na mtandao wa kijamii wa Twitter mwezi Mei mwaka huu.

Leave A Reply