The House of Favourite Newspapers

Rais Samia Amwagiza DCI kufanya Upelelezi Kabla ya Kumweka Mtu Mahabusu

0
Rais Samia akisalimiana na Viongozi wa Jeshi la Polisi

RAIS Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Agosti 30, 2022 amemtaka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai kuhakikisha anafanya upelelezi kabla ya kumuweka mtu mahabusu kwa kosa lolote alilotenda.

 

Rais Samia ameyasema hayo leo akiwa katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa Jeshi la Polisi kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yake.

 

Amempongeza DCI kwa hatua ambazo ameanza kuzichukua za kupunguza msongamano magerezani na kwenye vituo vya polisi huku akimtaka kufanya upelelezi kwanza kabla ya kumweka mtu ndani.

 

“Kabla ya kumpeleka mtu ndani, hakikisha umefanya kazi yako vizuri, una ushahidi wa kutosha ndiyo unakwenda kumsweka ndani. Lakini umemkamata, hujapeleleza, umeambiwa tu huyo msweke huko ndani.

 

“Huo ni mzigo kwa serikali na mzigo kwa familia. Sasa, tuyaangalie vizuri haya…wanachotaka wananchi ni kuona haki inatendeka haraka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zetu zilizowekwa,” amesema Rais Samia.

 

Amesema taarifa ya polisi imebainisha kwamba kesi 1,840 za watu waliokuwa magerezani zimefutwa kwa sababu ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha, jambo ambalo amesema limewaumiza watu hao.

 

“Tumepewa taarifa hapa kwamba kesi 1840 zimefutwa, hazikuwa na ushahidi wa maana, polisi tu katumia karma yake na nguvu yake, kamata twende peleka. Na pengine ukute aliyepelekwa kakataa kutoa kitu kidogo.

 

“Au mmegongana nyumbani huko, unamtafutioa angle huko, unambambikia kosa. Hawa ni wanadamu, hatujui wamekaa ndani muda gani, watu 1840, serikali inalisha, jamaa zao kiguu na njia kupeleka chakula, akiumwa kuhangaika,” amesema Rais Samia.

 

Awali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura alibainisha kwamba kesi 1,844 ziliondolewa mahakamani baada ya kuanza kwa mapitio ya kesi zote za watu waliokuwa magerezani na kesi 2,117 zimefikishwa Mahakamani na sasa ziko kwenye hatua ya kusubiri vikao vya Mahakama Kuu ili ziweze kusikilizwa

 

“Tumekubaliana kufanya kaguzi za pamoja kuanzia ngazi ya taifa, mikoa na wilaya ili kupunguza mlundikano wa mahabusi magerezani,” amesema IGP Wambura wakati akizungumza kwenye mkutano huo.

 

Leave A Reply