The House of Favourite Newspapers

Rais Samia na Uchumi wa Gesi, Adai Tupo Njia Sahihi na Salama

0
David Kafulila Mkuu wa Mkoa wa Simiyu

JUNI 11, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia makubaliano ya awali ya uwekezaji wa Dola Bilioni 30 kati ya Serikali yake na kampuni kubwa 5 za kimataifa ambazo ni Equinor, Shell, ExxonMobil, Medco Energy na Pavilion.

 

Hii ni hatua muhimu sana kuelekea makubaliano ya msingi kuhusu utekelezaji na uendeshaji wa mradi (Host Government Agreement) ambayo yanatarajiwa kufikiwa Disemba, 2022 na hatimaye maamuzi ya mwisho wa uwekezaji yanayotarajiwa kufikiwa mwaka 2025.

 

Huu ni uwekezaji mkubwa sana mashariki na kusini ya Afrika. Prof. Benno Ndulu mwaka 2016 alisema uwekezaji wa awali tu (initial investment) ungeongeza asilimia 2% ya pato la Taifa.

 

Uwekezaji wa $30bn ni karibu sawa na nusu ya uchumi wa Tanzania kwa sasa ($64bn), ni karibu sawa na uchumi wa Uganda kwa sasa($34bn), ni karibu mara 3 ya uchumi wa Rwanda kwa sasa ($11bn) na ni karibu sawa na theluthi moja ya uchumi wa Kenya kwa sasa ($99bn).

 

Kama mwenendo wa uchumi utaenda kama ulivyo (ceteris peribus), biashara hii itaifanya Tanzania kinara wa uchumi Afrika Mashariki.

 

Huu ni mradi mkubwa unaohusisha weledi katika maeneo mengi ya Nishati, Biashara na Uchumi wa kitaifa na kimataifa, sheria za kitaifa na kimataifa, mazingira na taalumu nyingi zinazohitaji weledi na uzoefu mkubwa. Ndiyo maana nilipata kuandika kwenye gazeti la Raia Mwema – Mei 05, 2021 kwamba tulihitaji mshauri eneo hilo kumudu meza ya majadiliano.

 

Ndiyo sababu niliposoma January 25, 2022 kuwa Serikali imepata mshauri mwelekezi kampuni ya yenye uzoefu ya Boots Barker kutoka Uingereza, nilipongeza nikiamini ilikuwa hatua muhimu sana kutanzua mkwamo wa mradi huu ambao ulifika mahala kuzua maswali ‘tunakwama wapi’ hasa ikizingatiwa nchi kama Msumbiji ilikuwa imepiga hatua mbele.

 

Ni kweli nchi yetu inawasomi na vyuo vingi lakini ni ukweli usiopingika kuwa hatuna hazina yenye weledi na uzoefu wa kutosha kwenda mezani mwanzo mwisho kwenye mradi mkubwa kiwango hiki bila kujengeana uwezo wa ziada.

 

Na kwa dunia ya leo siyo aibu kununua au kukodi utalaamu usiokuwa nao kufanikisha jambo kubwa kama hili. Nakumbuka Uingereza baada ya mgogoro wa kiuchumi walimteua Mark J. Carney ambaye alipata kuwa Gavana wa Canada kuwa Gavana wa Bank Kuu Uingereza ( NewYork Times – Nov26, 2012).

https://www.nytimes.com/2012/11/27/business/global/canadian-to-lead-bank-of england.html#:~:text=LONDON%20%E2%80%94%20In%20a%20surprising%20departure,Britain’s%20most%20prominent%20public%20officials

 

Au, mwaka wakati Uingereza inafanya maamuzi ya kujitoa Umoja wa Ulaya, walimteua mshauri mwelekezi kutoka New Zealand kuwa mshauri mwelekezi kwenye mikataba mipya ambayo Uingereza ilipaswa kuingia upya baina yake na mataifa mengine.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Alipoulizwa Waziri mkuu wa Uingereza kwa nini amefanya maamuzi ya kuteua mtaalamu kutoka nchi nyingine kuongoza timu ya wataalamu wake katika kushauri serikali kuhusu mikataba kati ya nchi yake na nchi zingine, alijibu kuwa kwa muda Uingereza imekaa Umoja wa Ulaya imepoteza uzoefu wake katika kuingia mikataba hiyo kwa kuwa miaka yote mikataba hiyo ilifanyiwa kazi Brussels.

 

Sasa kama taifa kubwa kama la Uingereza lenye vyuo bora duniani kuna mahala linakubali kupungukiwa na kukodi au kuazima utaalamu toka nje, sioni tatizo kwa nchi yetu. Muhimu ni kuwa tunajua tunachokitaka na hivyo mshauri anatusaidia namna ya kukifikia.

 

Lakini pia mradi kama huu unahitaji uelewa na uvumilivu kwa sababu ni mradi unaokwenda kubadilisha kabisa uchumi wa Tanzania ingawa inachukua muda (game changer). Ndiyo unaona mpango wa kufikia maamuzi ya uwekezaji unapangwa kufikiwa mwaka 2025 (investment decision), na mwanzo wa ujenzi mpaka kukamilisha itachukua miaka kadhaa pia. Na hii ni kawaida, nchi kama Canada iliwachukua miaka 7 kufikia maamuzi ya uwekezaji (Investment Decision) na kampuni hizi za kimataifa kwenye mradi kama huu wa Kitimat wenye thamani $31bn soma gazeti la CITIZEN – November8, 2018 hapa-

https://www.thecitizen.co.tz/tanzania/magazines/canada-offers-lessons-on-lng-project-for-tanzania-2661110

Kwenye dunia ambayo nishati ni mwamuzi wa uchumi duniani, makubaliano yake yanachagizwa na misukumo mingi ikiwemo ujasusi mkubwa kwani mafanikio ya nchi yoyote kuingia soko la LNG yanabeba tafsiri pia kwa nchi washindani ambazo zina sura tofauti ama za kama kampuni za kimataifa zinazoshindana au nchi wahusika zinazoshindana. Ndiyo sababu si ajabu tena mbinu kama ugaidi kuweza kuwa sehemu ya mkakati katika kukabiliana kibiashara tofauti na dhana ya zamani kuhusu misingi ya ugaidi.

 

Ni katika msingi huo uwekezaji mkubwa kama huu unachukuliwa tahadhari zote. Wote tunakumbuka kilichotokea Msumbiji baada ya kuonekana wanaweza kuingia mapema kwenye soko la LNG wakiwa na LNG ya bei nafuu sana kutokana na mazingira ya gesi yao asilia.

 

Msumbiji wana bahati kubwa ya gesi asilia karibu futi za ujazo trilioni 100 karibu mara mbili ya Tanzania ambapo gesi iliyokwishanguliwa inafikia futi za ujazo trilioni 57.

 

Zaidi, gesi ya Msumbiji karibu asilimia 85% inapatikana kwenye eneo la kina kifupi (shallow water) kulinganisha na Tanzania ambayo karibu asilimia 90% ya gesi ipo bahari ya kina kirefu (deepsea).

 

Niliwahi kugusia hili kama sababu ya Msumbiji kututangulia wakati bei ya gesi asilia dunia imeanguka kiasi ambacho ilihitajika kuzalisha kwa unafuu ili kuweza kuwa biashara.

 

Tafiti zinaonesha kwamba gharama za kuchimba kisima cha gesi kwenye kina kirefu (deapsea) ni karibu mara mbili ya gharama za kuchimba kina kifupi. Kwa takwimu za mwaka 2015 ni kati ya $50m- mpaka $70m kulinganisha na kisima kirefu (deap sea) ambacho ni kati ya $ 100m mpaka $120m.

https://www.sciencedirect.com/topics/engineering/drilling-cost

 

Naam, changamoto ni nyingi lakini tupo kwenye mstari sahihi. Tunahitaji kujenga mjadala wa uelewa ili kurahisisha mijadala kwenye masuala makubwa yenye maslahi mapana kwa Taifa letu leo na kesho. Tulipoamua kujenga uchumi wa gesi Tanzania, kwa kiasi kikubwa tulitazama mradi huu wa gesi asilia (LNG).

 

Leave A Reply