The House of Favourite Newspapers

Rais wa Vietnam Awasili Nchini

0

11

  Rais wa Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang (kushoto) pamoja na mkewe Bi. Mai Thi Hanh wakiwasili viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam, leo Machi 9, 2016 kwa ajili ya mazungumzo ya kuendeleza mahusiano katika nyanja mbalimbalikati ya Tanzania na Vietnam.

14

Mke wa Rais wa Vietnam, Bi. Mai Thi Hanh akipokea zawadi ya ua toka kwa mtoto mara alipowasili viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

17

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli (wa pili kushoto) akimkaribisha mgeni wake Rais wa Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang Ikulu Jijini Dar es Salaam.

20

Rais wa Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang (wa pili kulia) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (mwenye koti la drafti) mara alipowasili viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais Magufuli.

25

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli (kulia) pamoja na mgeni wake Rais wa Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang wakiwa katika jukwaa kwa ajili ya kuimbiwa nyimbo za Taifa kabla ya kukagua gwaride, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

31

 Rais wa Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang (mwenye tai nyekundu) akikagua gwaride la heshima katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam, Machi 9, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watanzania kujifunza kutoka kwa Vietnam namna ambavyo wameweza kupambana na umaskini kwa muda mfupi.

Mhe. Rais aliyasema hayo leo Ikulu katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mhe. Truong Tan Sang baada ya kusaini mkataba wa kukuza uhusiano baina ya Tanzania na Vietnam.

“Tanzania tunatakiwa tujifunze mambo mengi kutoka kwa wenzetu Vietnam ambao walipata uhuru mwaka 1945 wakaingia kwenye mapigano mpaka mwaka 1976. Wakati huo pato la muvietnam  mmoja lilikuwa dola 100 lakini leo ni dola 2000 na wamepunguza umaskini kwa asilimia 50 kuifanya nchi hiyo kuwa ya kipato cha kati,” alisema Mhe. Rais

Mhe. Rais Magufuli aliongezea kuwa, mwaka 1976 Vietnam ilichukua mbegu ya korosho kutoka Tanzania na kwenda kulima kwao, zao hilo limekuwa likifanya vizuri kwa nchi yao na wanaongoza kwa kulima korosho Duniani. Kwa upande wa Tanzania zao hilo limekuwa likitelemka chini kila mwaka.

Vilevile, Mhe Rais alisema kuwa Vietnam ni nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa samaki lakini Tanzania ambayo ina maziwa 21 pamoja na mito na bahari kila mahali haijaweza kuifikia Vietnam kwa uzalishaji wa samaki hivyo lazima watanzania tujifunze na tusiogope kujifunza ili Tanzania itoke mahali iliko.

Aidha Mhe. Rais alisema ziara ya Vietnam imekuja wakati muafaka wa kujenga mahusiano mazuri kwa watanzania na nchi ya Vietnam lakini hasa katika uchumi ili Tanzania iweze kufanikiwa namna ambavyo wao wamefanikiwa.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Truong alimshukuru Rais Magufuli na watanzania kwa mapokezi mazuri na ameahidi kuimarisha  mahusiano ya nchi hizi mbili hasa katika sekta ya kilimo, biashara, mawasiliano pamoja na uwekezaji.

Mhe. Rais Truong Tan Sang ni Rais wa kwanza wa nchi ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam kufanya ziara nchini Tanzania. Rais huyo ameambatana na mawaziri wanne pamoja na wafanyabiashara wapatao 30.

Mahusiano ya Tanzania na Vietnam yalijengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi wa Vietnam, Ho Chi Minh kuanzia mwaka 1960 na kupelekea kuanzishwa rasmi kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1965

Leave A Reply