MADRID, Hispania: MIEZI kadhaa iliyopita, kuna wengi waliombeza Cristiano Ronaldo wakati akipitia kipindi kigumu cha ukame. Ni Ronaldo huyohuyo ambaye aliibuka ghafla na kwenda kuipa Real Madrid ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga.
Msimu huu pia, Ronaldo, 33, aliuanza kwa tabu, wengi wakaanza kuibua maswali tena juu ya kiwango chake, lakini baada ya muda hakuna anayehoji tena.
Lakini ukweli ni kwamba huenda kizazi hiki tunamshuhudia mchezaji bora zaidi wa wakati wote katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mashabiki Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Juventus, walishuhudia kila kitu kwa uwazi zaidi. Baada ya Ronaldo kupiga bao la pili kali (Real ilishinda 0-3 ugenini), i l i b i d i mashabiki wa upinzani wasimame tu kumpa heshima kutokana na jinsi bao hilo lilivyokuwa.
“Sikuamini. Nalazimika kusema asante kwa mashabiki wote wa Juventus. Walichokifanya kwangu kinashangaza. Hii haijawahi kutokea katika maisha yangu,” alisema Ronaldo, baada ya mashabiki wa Juventus kusimama na kumpongeza kufuatia bao kali aliloifunga timu yao.
Suala la mchezaji bora zaidi litaendelea kuwa mjadala milele kwa kuwa ni mtazamo wa mtu. Kila mtu huwa na chaguo lake; mweupe au mweusi? Chapati au mandazi? Vitumbua au sambusa? Kunyoa au kufuga rasta?
Lakini kwa kile ambacho alikifanya Ronaldo Jumanne, inawezekana wengi wakaanza kukubali kuwa huyu ni mchezaji mkali zaidi kihistoria katika michuano hii.
Takwimu zinambeba: Yeye binafsi tangu aondoke kwenye Premier, amefunga mabao mengi kwenye michuano hiyo kuliko jumla ya mabao yaliyofungwa na timu mbili za Manchester United na Manchester City.
Kumbuka huyu ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa michuano hii, akiwa na mabao 120.
Bao lake la ‘tiki taka’ Jumanne, linasadikika kuwa ni bao bora zaidi lililowahi kufungwa katika historia ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa. Lilifungwa dhidi ya mmoja wa makipa bora zaidi wa wakati wote duniani, na lilifungwa licha ya jitihada za uhakika kutoka kwa safu ya ulinzi inayosadikika kuwa moja ya safu bora zaidi duniani, lakini jamaa akatupia tu.
Mtu aliyeshuhudia kwa ukaribu zaidi bao hilo ambaye alikuwa golini aliishia kumsifia tu. “Akiwa katika ubora wake? Nadhani hakuna aliyewahi kuwa kama Ronaldo. Messi na yeye (Ronaldo) wanaweza kulinganishwa na Maradona na Pele,” anasema Gianluigi Buffon, kipa wa Juve.
Hakika Ronaldo inaonekana alizaliwa kwa ajili ya kuja kufanya maajabu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata wakati akiwa na ukame kwenye La Liga, a l i e n delea kuwa hatari Ulaya msimu huu wa 2017-18.
Kwa mwendo wake huu wa kutupia mabao bila kuhurumia wapinzani wake, Ronaldo anaelekea kuvunja rekodi yake mwenyewe ya kufunga mabao 17 katika msimu mmoja, na kuna kila dalili kwamba atatwaa tuzo yake ya sita ya Ballon d’Or (Mchezaji Bora wa Dunia) kama Real Madrid itatwaa taji la Ligi ya Mabingwa kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Pia msimu huu ameweka rekodi mbili mpya: Jumanne alifanikiwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye mechi 10 mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya, na alifunga katika kila mechi kwenye hatua ya makundi, suala ambalo halikuwahi kufanyika kabla.
Ronaldo inawezekana akapata tena Tuzo ya Puskas, ambayo ni ya bao bora zaidi duniani, aliwahi kuipata mwaka 2009 baada ya kufunga bonge la bao katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya Porto.
Ronaldo anaelekea kubeba taji lake la nne la Ligi ya Mabingwa akiwa na Real Madrid, na la tano kwake kiujumla.
“Unyenyekevu ukizidi siyo vizuri,” alisema Ronaldo kabla ya fainali ya msimu uliopita. “Tunatakiwa kuthibitisha sifa yetu na tuwaonyeshe nani ni bora zaidi. Tunaweza kupata mataji mawili, kutetea ubingwa (wa La Liga) na kuingia katika historia ya Ligi ya Mabingwa. Kuna kichocheo kikubwa na tumebakiza hatua moja.”
Kuna hatua mbili na nusu zimebaki kwa ajili ya Madrid kugeuza mataji mawili mfululizo ya Uefa kuwa matatu mfululizo, lakini ugwiji wa Ronaldo katika michuano hii, umeshathibitishwa hata kama hawatatwaa taji hili.
Comments are closed.