The House of Favourite Newspapers

Ray c, usipobadilika huna wa kumlaumu!

0

00301047-b58ba41202d313a9834230ea50e40135-arc614x376-w1200

KWAKO dada yangu uliyesumbua Tanzania kwa uwezo wako mkubwa wa kuimba na kukata vilivyo kiuno stejini, Rehema Chalamila ‘Ray C’. Mambo vipi?
Ukitaka kujua afya yangu mimi ni mzima, hofu ni kwako uliye mbali ya upeo wa macho yangu. Kitambo sijakuona. Nimekukumbuka leo kwa barua maana kutokana na ubize wa shughuli zetu, yaweza pita hata mwaka hatujakutana.
Madhumuni ya kukuandikia barua hii mbali na kukujulia hali, nina jambo! Si lingine bali ni kuhusu suala la madawa ya kulevya.

Dada yangu, dunia nzima inajua kwamba ulitopea kwenye hii kitu na inafahamu ulipitia kwenye mateso makubwa ulipokuwa ‘mteja.’
Afya yako ilizorota. Lakini tunashukuru Mungu si Athumani, Gazeti la Ijumaa ndilo lilikuwa la kwanza kukuokoa. Lilikuanika ulipokuwa umetopea kwenye madawa hayo hatari yanayoangamiza vijana wengi kwa sasa duniani.
Ukawa ndiyo mwanzo wa Watanzania kujua kwamba una matatizo. Waliokuwa wakifuatilia muziki wako tangu zamani nikiwa miongoni mwao, niliumia sana. Sikutarajia kukuona ukiwa kwenye hali kama ile ambayo ilikuwa ni ya hatari.

Kutokea hapo, Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alikuona. Akajitoa kukusaidia ili urudi kwenye hali ya kawaida. Kwa kusaidiana na wadau, wakakufikisha kwenye kitengo cha tiba ya waathirika wa madawa ya kulevya na ukaanza kupatiwa dawa.

Kinachonisikitisha ni kusikia umerudia tena kwenye utumiaji wa madawa hayo. Kwamba imefika wakati hadi unaleta fujo kwa madaktari wanaokuhudumia katika Hospitali ya Mwananyamala.
Kama hiyo haitoshi, mdau aliyepewa jukumu na rais kukusaidia naye ilifika wakati akachoka. Inasemekana ulianza kumletea jeuri. Ukawa husikii unachoelekezwa.

Jitihada za rais na za mdau zikawa zinaonekana kugonga ukuta. Ukawa unakwenda kuchukua dawa pale unapojisikia na wakati mwingine kuwaletea fujo madaktari wa pale Mwananyamala. Dada yangu hilo naliona ni tatizo ambalo lina ishara mbaya kwako.

Nasema ni ishara mbaya sababu itafika wakati hakuna atakayekuwa tayari tena kukusaidia. Bahati mbaya sana eti tulipokuwa tunaandika habari zako katika magazeti ya Global Publishers, ulikuwa unaibuka na kudai unaonewa.

Ukawa unatumia nguvu kubwa kukanusha katika mitandao ya kijamii. Ulifanya hivyo ukijua ukweli hauwezi kubainika lakini nikueleze tu, hayo ni maradhi. Hata ukificha vipi, utaumbuka tu kama ilivyokutokea hivi karibuni baada ya picha zinazokuonesha ukiwa ‘bwii’ kupatikana.

Nikushauri tu dada yangu, hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako achaana na madawa hao ili urudi kwenye ubora wako kimuziki, vinginevyo utaangamia. Mimi ni nduguyo;
Erick Evarist

Leave A Reply