The House of Favourite Newspapers

RC Geita Aipongeza GGML kwa Kuwajengea Uwezo Wafanyabiashara Wadogo

0
Mkuu wa mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Richard Jordinson (kushoto). Mkuu wa wa mkoa alitembelea GGML kwa mara ya kwanza na kujionesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo nchini.

 

 

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameupongeza uongozi wa Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu Geita- GGML kwa kushiriana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuanzisha mpango maalumu wa kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo mkoani humo kupata fursa za kibiashara katika mgodi huo.

 

Senyamule ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipotembelea mgodi huo kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo na kujionea shughuli mbalimbali za uchimbaji wa madini zinazofanywa na kampuni hiyo.

 

Akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na Wilaya ya Geita, Mkuu huyo wa mkoa alielezea furaha yake katika kujifunza jinsi GGML inavyofanya shughuli zake za uchimbaji pamoja na biashara kwa kufuata sheria na kanuni za serikali.

“Nimekuwa nikifuatilia taarifa za kampuni hii kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini ikiwamo tuzo mliyopata ya kuwa mlipa kodi mkubwa na kampuni inayoongoza kwa uchimbaji wa madini nchini kwa kuzingatia usalama na uhifadhi wa mazingira.

 

“Katika ziara hii ya kwanza ningependa kuipongeza GGML kwa  namna ambavyo mnafanyabiashara na wakati huo huo mkiendelea kutimiza majukumu ya uwajibikaji wa kijamii.

 

“Kuhusu programu ya kuwawezesha wajasiriamali wenyeji wa Geita kupata fursa za biashara kutoka GGML, hakika ni program ya kipekee ambayo napenda kuwapongeza kwa sababu inahimiza mazingira endelevu ya kibiashara hapa mkoani Geita. Ninashauri GGML kutekeleza miradi zaidi na yenye tija na ufanisi endelevu,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Akizungumzia mafanikio ya Kampuni hiyo katika kipindi cha miaka 21 iliyopita, Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya ubia, Manace Ndoroma alifafanua namna GGML imejitolea katika nyanja mbalimbali ikiwamo maendeleo endelevu kwa jamii inayozunguka mgodi.

 

“Tumeendelea kuonyesha dhamira ya uwekezaji kwa kijamii kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na barabara pamoja na shughuli zingine za kiuchumi kwa jamii inayozunguka mgodi.

 

“GGML imetumia zaidi ya Sh bilioni 30 kutekeleza miradi kadhaa ya jamii kwa kushirikiana na serikali za mitaa za Geita baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini mnamo 2017,” alisema.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply