The House of Favourite Newspapers

Rich Mavoko Ndiye Aliyemtoa Mbosso Baada ya Kukata Tamaa ya Muziki

0
Msanii wa Bongo Fleva, Rich Mavoko

Msanii wa Bongo Fleva, Rich Mavoko, kumbe ameshatengeneza ngoma kubwa za kutosha na anahesabika kuwa ni miongoni mwa waimbaji wazuri Tanzania, kwani ameshatoa albamu na EP.

Ni msanii ambaye amefanya kolabo za kimataifa, kwa kifupi ana historia yake ndani ya Bongo Fleva.

Unachotakiwa kujua ni kwamba Rich Mavoko ndiye alienda nyumbani kwa msanii Mbosso na kumchukua hadi Sinza zilipokuwepo ofisi za Wasafi Classic Baby (WCB) kwa wakati huo na ndipo siku hiyo Mbosso alisaini mkataba wa kuwa chini ya lebo hiyo.

Mbosso alikuwa ameshakata tamaa ya muziki ila Mavoko alikuwa anamtia moyo kila walipokuwa wanakutana katika mazoezi ya mpira.

Msanii wa WCB, Mbosso.

Kabla ya Rich Mavoko kusaini WCB hakuwahi kukutana au kuongea na mmiliki wake ambaye ni Diamond Platnumz ‘Mondi’ kuhusu hilo, kumbe AY ndiye aliyemkutanisha na Sallam SK wakiwa nchini Uganda kwenye shoo ya msanii maarufu nchini humo, Jose Chameleone ndipo yalipoanza mazungumzo ya kujiunga na lebo hiyo.

Rich Mavoko aliwaandikia ubeti wa mwisho (verse) ya wimbo wa Malaika, ‘Rarua’ na ndio ngoma iliyofanya vizuri hadi Malaika kupata ‘Tour’ Washington DC, Marekani mwaka 2017.

Lakini pia Lulu Diva alimshirikisha Rich Mavoko baada ya kumlipa fedha ili kumshirikisha katika wimbo wake ‘Ona’ licha ya kudaiwa ni wapenzi.

Video ya wimbo huo ndio video ya pekee ya Lulu Diva iliyofikisha watazamaji (views) zaidi ya milioni moja kwenye mtandao wa YouTube.

Pia wimbo wa ‘Sijaona’ ambao ni wa tisa kutoka kwenye albamu ya Diamond Platumz ‘A Boy From Tandale’ umeandika na Rich Mavoko wakati huo akiwa chini ya lebo ya Wasafi Classic Baby.

Jambo la kipekee kwa Rich Mavoko ni kwamba licha ya kutokea Morogoro, hajawahi kuutaja mkoa huo katika nyimbo zake kama wasanii wengine wanavyofanya.

Kuna jambo ambalo mashabiki wake wanajiuliza na hawajapata jibu kwamba kwa nini video za nyimbo zote ambazo Rich Mavoko alizitoa chini ya WCB Wasafi kama ‘Kokoro’, ‘Rudi’ na ‘Imebaki Stori’ zimeondolewa kwenye majukwaa ya kidijitali kama vile mtandao wa YouTube?

Rich Mavoko anafanana kitabia na Mwana FA hasa kuhusu mahusiano yake na ni msanii ambaye hapendi sifa.

Mwana FA hapendi pia kukaa na wasichana wenye kujipendekeza kwa jamii ili kupata sifa.

Rich Mavoko amefanya kolabo na wasanii wengi nchini na Fid Q ndiye msanii wa Hip Hop Bongo aliyefanya kolabo nyingi zaidi na msanii huyu. Wawili hao wameachia ngoma nyingi kama ‘Sheri’, ‘Blow Up’, ‘Tawile’, ‘Champion’ na ‘Bambam’.

Rich Mavoko amewahi kuwa mwanasoka na kama sio muziki basi angekuwa mcheza soka, kwani shuleni alicheza pamoja na mchezaji wa Azam FC, Frank Domayo, Mavoko alicheza namba nane ila kutokana na ufupi wake mwalimu akamuhamishia namba saba.

Mavoko aliwahi kujiunga na WCB lakini baadaye akajiondoa.

Taarifa za Mavoko kutemana na WCB zilianza kutrend kama utani vile, ambapo Gazeti la Ijumaa lilikuwa  likifuatilia hatua kwa hatua baada ya tetesi kusambaa kwa kasi.

Juni 19, mwaka 2018 Diamond alizungumza na waandishi wa habari ambapo wasanii wote wa WCB walikuwepo isipokuwa Mavoko.

Lakini, meneja wa Mond, Babu Tale alipoulizwa kutokuwepo kwa Mavoko akadai kuwa alikuwa amebanwa akifanya video ya wimbo wake mpya hivyo, asingeweza.

Hata hivyo, wasanii wa WCB wamekuwa na kawaida ya kushirikiana kama siafu pindi wanapokuwa na ngoma mpya ambapo wamekuwa wakivamia kwenye mitandao ya kijamii kutangaza kazi za msanii mwenzao, jambo ambalo limekuwa likiwapa mafanikio makubwa.

Leo Mavoko yupo nje ya WCB na alipowahi kuulizwa anaona utoauti gani kuwa peke yake na kuwa ndani ya WCB, Mavoko aliwahi kukiri kuwa akiwa ndani ya WCB alikuwa na wakati mzuri zaidi kwani alichotakiwa kufanya ni kuandaa ngoma kali tu na kupanga jinsi ya kuwika.

Lakini sasa yupo nje, inabidi awaze yote yeye mwenyewe jinsi ya kufanya nyimbo na jinsi ya kufanya promosheni ya nyimbo hizo ili ziwike.

Na Elvan Stambuli, Gazeti la Ijumaa

FEI TOTO NDIYO BASI TENA, YANGA NA SIMBA WATAUANA | KROSI DONGO….

Leave A Reply