The House of Favourite Newspapers

Rigobert Song; Shujaa wa Cameroon Mwenye Rekodi Zake AFCON

rigobert-song

HUWEZI ukazizungumzia rekodi za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) bila kulitaja jina la Mcameroon, Rigobert Song (pichani). Jamaa ana rekodi kibao kwenye michuano hiyo pamoja na nchini kwao Cameroon kwa ujumla.

Rigobert Song Bahanag, aliye­zaliwa Julai Mosi, 1976, alikuwa mchezaji wa Cameroon kwa miaka 17 kuanzia 1993 hadi 2010.

Akijulikana duniani kote kutokana na uwezo wake wa kukaba, Song, 40, mara nyingi alicheza kama beki wa kati lakini aliweza pia kucheza kama beki wa kulia kwa ustadi mkubwa.

Rekodi ya kwan­za aliyonayo Afcon ni kwamba, alicheza kwenye michuano nane ya Afcon huku akiwa na­hodha katika michuano mitano (michuano am­bayo hakuwa nahodha ni ya Afrika Kusini 1996, Burkina Faso 1998 na 2010). Hakuna mchezaji mwingine aliyewahi kufanya hivyo.

rigobert-song-na-etooSong akiwa na Samuel Et’oo mazoezini

Song pia anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi mfu­lulizo katika Afcon. Alicheza mechi 35 mfululizo katika kikosi cha kwanza cha Cameroon. Pamoja na hayo, alitwaa ubingwa wa Afcon mara mbili; 2000 na 2002.

Mwaka 2009, Song alistaafishwa unahodha na kocha mpya Paul Le Guen, ambaye alimpa kitambaa hi­cho Samuel Eto’o, baadaye kocha huyo akaishangaza Cameroon kwa kumuweka benchi Song ambaye kabla, hakuwahi kuwekwa benchi kwa miaka 11 akiitumikia Cam­eroon.

Akiwa ameichezea C am­eroon mechi 137, Song pia anashikilia re­kodi ya mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika historia ya timu ya taifa ya Cameroon na amecheza katika michuano minne ya Kombe la Dunia; 1994, 1998, 2002 na 2010.

rigobert-song

Song alianza maisha yake ya soka akiwa Metz na aliisaidia timu hiyo ya Ufaransa kutwaa taji la Kombe la Ligi (Coupe de la Ligue) mwaka 1996. Baada ya kutokeza kwenye Kombe la Dunia 1998, Song alijiunga na Salernitana, am­bayo ilikuwa imepanda kucheza Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Akiwa pamoja na Zinedine Zi­dane, Song ni mchezaji pekee ku­tolewa nje kwa kadi nyekundu kati­ka michuano miwili ya Kombe la Dunia, mara ya kwanza dhidi ya Brazil mwaka 1994 na mara ya pili dhidi ya Chile mwaka 1998. Pia anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kutolewa kwa kadi uwanjani kwenye Kombe la Dunia, alikuwa na miaka 17.

Song ambaye mashabiki Watu­ruki walimuita jina la utani la ‘Big Chief’, ni mjomba wa kiungo mkabaji Mcameroon anayeichezea Rubin Kazan ya Urusi, Alex Song.

Akiwa ni Mcameroon wa kwanza kuichezea Liverpool, Song alikuba­lika vilivyo kwa mashabiki wa klabu hiyo ambao walikubali nguvu zake, staili na juhudi zake na mara kad­haa walikuwa wakimwimbia: “Tuna Song mmoja tu.” Msimu wa 1999- 2000 alikosekana kwa miezi mitatu kutokana na majukumu ya timu ya taifa ambapo alikwenda kuiongoza Cameroon kutwaa ubingwa wa Af­con 2000 akiwa nahodha huku aki­funga penalti ya kuamua mshindi katika mchezo wa fainali dhidi ya Nigeria.

rigobert-song1Song alishuhudia mengi, moja­wapo ni kuwa katika michuano ya Kombe la Mabara 2003, mchezaji mwenzake Marc-Vivien Foé alian­guka uwanjani akimshuhudia na baadaye aka­fariki dunia na kuzua si­manzi kubwa duniani.

Katika Af­con 2008, Song aliiongo­za Cameroon hadi fainali lakini alifanya kosa kubwa lililozaa bao pekee la Misri lililofungwa na Mohamed Aboutrika na kuiko­sesha timu yake kombe. Wakati Wamisri wakishangilia, Song aliu­funika uso wake kwa jezi akilia kwa uchungu.

Baada ya hapo, Song aliendelea kufanya makosa mengi ya ajabu. Katika Afcon 2010, alifanya kosa lililosababisha Gabon wakapata bao na kushinda 1-0 lakini katika mchezo mwingine dhidi ya Zambia aliunganisha krosi kwenye goli lake mwenyewe. Timu ilifika robo fain­ali lakini ikatolewa kwenye dakika 30 za nyongeza na Misri.

Song alistaafu kuichezea Cam­eroon mwaka 2010 akiwa ameche­za mechi 137 na kufunga mabao matano. Kwa ngazi ya klabu pia alistaafu mwaka 2010.

rigobert-song4 MATAJI

FC Metz: Coupe de la Ligue: 1995-96. Galatasaray: Süper Lig: 2005-06, 2007-08, Turkish Cup: 2005. Trabzonspor: Turkish Cup: 2009, Turkish Cup: 2010. Cam­eroon: Afcon (2): 2000, 2002.

MAISHA BINAFSI

Baba yake Song, Paul Song, alifa­riki dunia wakati Song akiwa mtoto. Hamjui baba yake, lakini alikuwa akiyatoa mabao yake kwake. Song amemuoa mrembo Esther Song na wana watoto wanne. Hivi sasa wanaishi Liverpool. Song alipata shambulio la moyo Oktoba 3, 2016 na alilazwa Cameroon. Alipoteza fahamu kwa siku mbili lakini mwis­honi mwa mwaka iliripotiwa hali yake imeimarika.

ANACHOKIFANYA KWA SASA

Hivi sasa Song ni kocha wa timu ya taifa ya Cameroon ‘A’ ambayo ni ya wachezaji wa­naocheza ndani ya Cameroon.

song-1475662858

 KLABU ALIZOCHEZEA

MWAKA KLABU MECHI MABAO

1994-1998 Metz 123 3

1998-1999 Salernitana 4 1

1999-2000 Liverpool 35 0

2000-2002 West Ham 28 0

2001-2002 Köln (mkopo) 19 1

2002-2004 Lens 75 4

2004-2008 Galatasaray 126 6

2008-2010 Trabzonspor 56 2

JUMLA 466 17

Kwa stori zote kali, Tu-follow

Facebook @Globalpublishers

Twitter @GlobalHabari

Instagram @GlobalPublishers

YouTube @GlobalTVTZ

Endelea kutembelea website ya Global Publishers kila siku, tutaendelea kukusogezea kila news inayotokea mahali popote duniani.

Shinda Nyumba Awamu ya Pili Yatikisa Jiji la Dar es Salaam

Comments are closed.