The House of Favourite Newspapers

Ripoti Kifo cha Akwilina Kizungumkuti, Ndugu Wagoma Kuchukua Mwili

Mkuu wa Chuo cha NIT, Zakaria Mganilwa.

 

RIPOTI maalum ya uchunguzi kuhusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini imezua kizungumkuti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ulipohifadhiwa baada ya ndugu wa marehemu kuelezwa kuwa majibu ya ripoti hiyo yatatolewa baada ya siku 14 huku baadhi yao wakipinga jambo hilo na kutaka wapewe leo.

 

Wakizungumza na Global TV Online leo Februari 19, 2018 baada ya postmortem ya uchunguzi huondugu wa Akwilina waliokuwa wamekusanyika Muhimbili karibu na eneo la chumba cha kuhifadhia maiti wakisubili ripoti, wameeleza kusikitishwa kwao na uamuzi huo huku wakilalamika na kuhoji kwa nini wasipewe ripoti hiyo leo ili wakazike mwili wa ndugu yao.

 

“Tumeambiwa na daktari tayari uchunguzi umeshakamilika, tuchukue mwili tukazike, lakini wanasema majibu yatatoka baada ya siku 14. Hivi tukienda tukizika tutawaambiaje waombolezaji na ndugu wengine, kwamba ndugu yetu alikufa je?” alisema ndugu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake litajwe.

 

Hali hiyo ilizua sintofahamu huku wengine wakikubali kuchukua mwili na wengine wakikataa wakitaka kupewa ripoti kamili ya uchunguzi wa kifo hicho. Mpaka tunaenda mitamboni bado mjadala wa kuchukua  mwili huo ulikuwa unaendela Muhimbili na maridhiano baina ya ndugu yalikuwa hayajapatikana.

 

Kwa upande wa Mkuu wa  NIT, Prof. Zakaria Mganilwa amesema uongozi wa chuo hicho umeungana na familia kuhakikisha wanampumzisha Akwilina huku akifanya jitihada za kuzungumza na madaktari na ndugu wa marehemu kufanikisha zoezi la kuchukua mwili na kwenda kuuzika.

 

“Ripoti juu ya kifo chake madaktari wanasema itakuwa tayari baada ya siku 14 hivyo wakawa wamewaruhusu ndugu kuchukua mwili huo ili wakazike lakini ndugu wa marehemu wanasema hawawezi kuchukua mwili mpaka wajue yaani ripoti itoke ndiyo waweze kuchukua mwili kwa hiyo bado wanaendelea kufanya majadiliano na mamlaka husika,” alisema Profesa Zacharia.

Mnamo Februari 16, 2018 Akwilina alipigwa risasi akiwa kwenye daladala ambayo inasemekana ilikuwa inapita eneo ambalo polisi walikuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA ambao walikuwa wakielekea kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi Kinondoni. 

VIdeo: Msikie hapa akizungumza

Comments are closed.