The House of Favourite Newspapers

RITA UMEMHUZUNISHA CASSIAN; UMEJIVUNJIA HESHIMA

Rita Paulsen

MIAKA takriban mitatu nilipozun-gumza na mwanadada Rita Paulsen nilimwambia thamani yake mbele ya jamii. Nikamtia moyo kwa kumwambia azidi kusonga mbele.  

 

Mazungumzo yetu yalikuwa ni kuhusu shindano lake la Bongo Star Search ‘BSS’ ambalo lilionekana kuanza kupigwa zengwe na wabaya wake. Huyu ndiye mimi; wanaonifahamu si mpindisha ukweli; chokaa kwangu haitafananishwa na maziwa hata kama vyote ni vyeupe.

 

Nikiwa na heshima ile niliyompa dada yangu Rita tangu zamani, hivi karibuni nikasoma habari moja kwenye gazeti linalotoka kila siku (si la Global) ikinukuu maneno ambayo mpaka sasa siamini kama aliyatamka yeye au alilishwa.

 

Kwamba, hawezi kumsaidia gharama  za matibabu Mshindi wa BSS 2009, Paschal Casian kwa kushinikizwa na watu na kwamba msanii huyo ambaye kwa sasa ni Muimba Injili hawadaiani kitu chochote kwa sababu walishalipana stahiki tangu miaka 9 iliyopita.

 

Kwa msingi huo haoni sababu ya kulazimishwa na watu kumsaidia kumtibu kijana huyo ambaye alipata ajali mbaya ya gari mapema mwaka jana na kuharibika kibofu cha mkojo. Alikaririwa akisema hana fedha za kumtibu na kwamba naye ana majukumu katika familia yake, akafika mbali zaidi kwa kusema hao wanaompigia kelele za kumtaka amsadie Cassian wamtibu na wao kwa sababu yeye amemsaidia katika mengi.

 

Najiuliza; Rita huyu ambaye anafungua njia ya mafanikio ya vijana kwa kuwasaidia kutambua vipaji vyao anaweza kutamka maneno makali namna hii kwa kijana ambaye amepita kwenye ulezi wake? Kama ni yeye, amepatwa na kitu gani mpaka kufikia kupoteza imani na huruma kiasi hicho?

 

Nakumbuka habari ya kwanza kabisa kuhusiana na Cassian kulazwa Hospitali ya Muhimbili iliandikwa na vyombo vya habari vya Global, ikiwemo Global TV Online. Hata kauli ya kuomba Madam Rita amsaidie Cassian aliitoa kwa waandishi wa Global na mimi ndiye niliyeipitia stori ikatoka.

Katika maelezo ya Cassian hakuna mahali alipomlaumu Rita kwa chochote, badala yake kwa mapenzi na imani yake alimuomba kama ndugu asikiapo matatizo yake amsaidie kwa lolote, nakumbuka alisema; “Rita ana watu wengi” akiamini kabisa hawezi peke yake kumsaidia kwa asilimia mia na akapona.

 

Leo hoja inapotolewa kwamba analazimishwa na watu amtibu nashangaa; kwani Cassian aliwatuma hao watu waandike kwenye mitandao ya kijamii wamshurutishe amtibu?

 

Kama hakuwatuma, kwa nini Rita amepoteza huruma kwa Cassian na kumtolea maneno hayo mazito? Ukisikia kuweka dhahabu kwenye pua ya nguruwe ndiko huku, kwamba lazima itageuka tope na kweli Cassian kawa tope. Watoka mila zinazojali maadili; mtu kukueleza ugonjwa wake sambamba na kuja kukulilia shida ni kukuheshimu sana.

 

Sitaki kuamini kwamba kwa umaarufu wake wote alionao Cassian hana watu wengine wa kuwapelekea shida zake; wapo wachungaji, waimba injili wenzake lakini aliwaacha wote akampa heshima bosi wake wa zamani Rita. Ingepaswa kabisa heshima hiyo Rita aipokee na kuilinda hata kama mfukoni hana kitu. Lakini anapomnanga Cassian kwamba hawadaiani ni kumhuzunisha na kumpotezea tumaini la kuishi.

 

Tangu lini mgonjwa akaelezwa maneno makali ya kukatisha tamaa? Pole Cassian unapaswa kufarijiwa hata kwa maneno ya uongo katika kipindi hiki kigumu ulicho nacho kuliko kuvunjwa moyo. Ushauri wangu mwingine kwa Rita leo ni kumuomba radhi Cassian kwa sababu amemkosea na kibaya zaidi makosa hayo yamemvunjia pia heshima yeye kama kioo cha jamii.

 

Tangu aanzishe Shindano la BSS amejipatia sifa nyingi kwamba ameweza kuwasaidia vijana wengi kujiajiri na kufungua milango ya mafanikio yao. Kama si yeye nani angemjua Cassian, kama si BSS akina Jumanne Idd, Kala Jeremia, Peter Msechu na Kayumba wangekuwa wapi leo?

 

Naamini Rita hajapotea njia, ameteleza na kwamba anatakiwa kuambiwa na makala haya kwamba amevuka nguo; ajistiri ili aibu isiendelee kukaa naye. Mara nyingi nimekuwa nikiwashauri watu ambao wanaonekana kuwa ni miti yenye matunda katika jamii kama Rita kwamba kuna sehemu ukifika katika maisha ni vyema ukajifunza kuchunga ulimi ili usikuponze.

 

Kama hilo halitoshi kujitambua kwa ujumla ni jambo muhimu sana, ndiyo maana baadhi ya watu wakifika sehemu fulani hutafuta washauri na watu watakaokuwa na uwezo wa kuwasaidia kupangilia kipi cha kusema na cha kunyamaza. Kwa mfano, hata kama Rita amesemwa mitandaoni mara ngapi kuhusu Cassian ingemfaa kunyamaza kuliko kujaribu kujitakasa kwa ‘oil chafu’!

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO


Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.