The House of Favourite Newspapers

Robertinho Aanza Jeuri Simba Baada ya Kuwafunga Wydad Casablanca Kwa Mkapa

0
Kocha Mkuu Wa Simba Roberto Oliveira Maarufu Robertinho.

ROBERTO Oliveira maarufu Robertinho ambaye ni Kocha Mkuu wa Simba, amesema timu hiyo inacheza mchezo wa kisasa jambo linalowapa matokeo bora uwanjani.

Msimu huu, Simba imecheza mechi 19 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila kupoteza, mara ya mwisho ilifungwa 1-0 na Azam FC, mtupiaji akiwa Prince Dube. Ilikuwa Oktoba 27, 2022 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

Kwenye mechi nne mfululizo zilizopita ambazo ni dakika 360, Simba haijapoteza wala kupata sare, imeshinda zote. Ilikuwa ni Simba 5-1 Ihefu mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports hatua ya robo fainali, Ihefu 0-2 Simba mchezo wa ligi, Simba 2-0 Yanga mchezo wa ligi.

Wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 1-0 Wydad Casablanca, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali, hapo Robertinho amefikisha mchezo wa nne mfululizo bila kufungwa kwenye mechi za ushindani.

Akizungumza na Spoti Xta, Robertinho alisema wanatambua namna ya kupambana na wapinzani wao kitaifa na kimataifa kutokana na mbinu za mpira wa kisasa kukubalika kwa wachezaji wake.

“Unaona ambavyo tunacheza kwenye mechi zetu, iwe za kitaifa na kimataifa, ni mtindo wa kisasa ambao tunatumia unatupa matokeo chanya, hili ni furaha kwetu.

“Pongezi kwa wachezaji kutokana na kujituma kwao na wanafanya kazi nzuri, ninawapongeza, bado tuna kazi nyingine kwenye mchezo ujao dhidi ya Wydad ambapo tutakuwa ugenini.

“Kwenye mpira kila kitu kinawezekana, ni suala la kusubiri na kuona hasa kwenye kutengeneza nafasi na kuzitumia, huu ni mchezo ambao unaangalia mpira upo na nani na atafanya nini kwa wakati huo,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.

STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA

HALIMA MDEE AIBANA SERIKALI AHOJI KUHUSIKA KWAKE UTAPELI wa MITANDAONI, NAIBU WAZIRI AJIBU…

Leave A Reply