The House of Favourite Newspapers

Robertinho Ataja Kinachoimaliza Simba Azungumza na Spoti Xtra…Soma Hapa

0
Kikosi cha Simba.

ROBERTO Oliveira ‘Robertinho’, Kocha Mkuu wa Simba, amesema wachezaji wa timu hiyo wanacheza kwa juhudi kubwa, lakini tatizo la kukosa umakini kwenye umaliziaji wa nafasi, ndilo linalowamaliza.

Timu hiyo imetoka kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa juzi Jumanne, kituo kinachofuata ni dhidi ya Vipers ikiwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Jumamosi hii nchini Uganda.

Simba katika mechi tatu zilizopita za michuano yote, imepoteza mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na kupata sare moja kwenye Ligi Kuu Bara.

Ikumbukwe kuwa, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inaongozwa na Jean Baleke, John Bocco, Kibu Denis, Ousmane Sakho na Moses Phiri.

Kocha Mkuu wa Simba, ROBERTO Oliveira ‘Robertinho’.

Akizungumza na Spoti Xtra, Robertinho alisema kila: “Kuna makosa ambayo tunayafanya hasa kwenye eneo la umaliziaji, ile miguso ya mwisho ambayo tunatengeneza tunashindwa kuitumia, kuna wachezaji wazuri wenye vipaji ikiwa ni pamoja na Habib Kyombo, Sadio Kanoute, Shomari Kapombe, Jonas Mkude na Clatous Chama.

“Sio hao tu, bali wachezaji wote kwenye kikosi cha Simba wanafanya kazi nzuri na wana uwezo mkubwa ukizingatia kwamba Simba ni timu kubwa, tunaamini tutafanya vizuri mechi zijazo.

“Tunafahamu mbele yetu kuna mchezo mgumu dhidi ya Vipers na sio rahisi kwetu kucheza michezo yote hii kwa ratiba tuliyonayo na ikizingatiwa ndiyo kwanza nina miezi miwili pekee hapa, hivyo tunatarajia kufanya mabadiliko kidogo ya kikosi kuelekea mchezo huo ambao ni muhimu kushinda.”

Kuhusu sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam, Robertinho alisema: “Sikuitegemea kabisa hii sare ambayo tumeipata dhidi ya Azam, kutokana na idadi ya nafasi za wazi ambazo timu yangu imezipata.

“Sio katika mchezo huo pekee, pia tumekosa nafasi nyingi katika michezo ya kimataifa dhidi ya Horoya na Casablanca, licha ya kuwapa mbinu nyingi za kufunga mabao washambuliaji wangu.

“Kufundisha washambuliaji jinsi ya kufunga sio kazi ndogo, lakini ninaendelea kuiboresha zaidi safu yangu ya ushambuliaji.”

STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA NA WILBERT MOLANDI

KUMEKUCHA! WAARABU WAIBEBA YANGA MALI, SIMBA IWE ISIWE VIPERS ANAKUFA KWAO | KROSI DONGO

Leave A Reply