The House of Favourite Newspapers

Ronaldo Aanza Kazi Kibabe, Apiga Mtu Mbili Italia

STAA wa Juventus, Cristiano Ronaldo, jana alianza kazi ya kutupia kwenye nyavu baada ya kuifungia timu yake ya Juventus mabao mawili kwenye Uwanja wa Allianz.

 

Ronaldo alikuwa amecheza michezo mitatu kwenye Ligi Kuu Italia, Serie A, bila kufunga bao lolote lakini jana alikuwa staa wa mchezo wakati Juventus ilipopata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sassuolo.

 

Ronaldo alifanikiwa kufunga mabao hayo katika dakika ya 50 na 65 na kuanza kasi ya kuwania kiatu cha ufungaji bora kwenye ligi hiyo, huku wageni hao wakijipatia bao moja katika dakika ya 90 kupitia kwa Khouma Babacar.

 

Staa huyo ambaye alipumzika wakati wa wiki mbili za michezo ya kimataifa, alitua Juventus mwanzoni mwa msimu huu akitokea Real Madrid.

 

Hata hivyo, Douglas Costa wa Juventus alipewa kadi nyekundu dakika za mwisho baada ya kumtemea mate mchezaji wa timu pinzani, ikiwa ni dakika chache baada ya kupewa kadi ya njano kwa kumpiga kichwa mpinzani, kisha kumpiga kiwiko.

 

Hii ni picha kuwa staa huyo ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita na mwenye tuzo tano za mchezaji bora wa dunia, anaweza kuanza kasi yake ya kutetea ukinara wake tena wiki hii.

MILAN, Italia

Comments are closed.