The House of Favourite Newspapers

ROSA REE AFUNGUKA MJENGO WAKE WA MILI. 400, KUMILIKI SUPERMARKET

MWANAMUZIKI wa kike anayekimbiza kwenye gemu la Muziki wa Hip Hop Bongo, Rosary Robert ‘Rosa Ree’ ambaye anapenda kujiita pia Rap Goddess, ‘ametrend’ kutokana na kutambulisha mjengo wake wa maana huko Tegeta jijini Dar unaodaiwa kuwa na thamani milioni 400.

Mbali na kutambulisha mjengo huo, Rosa Ree alitambulisha pia ngoma yake ya Way Up aliyofanya na mwanamuziki kutoka Afrika Kusini, Emtee sambamba na menejimenti yake mpya kutoka huko ‘bondeni kwa Madiba’ iitwayo Dimo Production.

 

Mwanadada huyo anakuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike Bongo kufikia mafanikio aliyonayo kwa kipindi cha miaka mitatu tu aliyodumu kwenye gemu toka mwaka 2015, alipoanza muziki rasmi huku wimbo wake wa kwanza wa One Time akiuachia Oktoba 2016.

Aliwahi kuwa kwenye Lebo ya The Industry inayomilikiwa na Kundi la Navy Kenzo, lakini baadaye aliondoka kwenye lebo hiyo. Katika mazungumzo haya na Mikito Nusunusu, amefunguka mambo mengi kuhusu maisha yake mapya ya muziki baada kusainiwa Dimo Production. Shuka naye;

Mikito: Tukianza na kazi mpya ni nzuri, hongera, lakini kwa nini Emtee na siyo mwanamuziki mwingine?

 

Rosa Ree: Ni Emtee, kwa sababu ni mwanamuziki mkali na kama unavyoelewa kufanya kazi na mwanamuziki wa nje ni lazima kuwe na ‘koneksheni’ lakini pia ‘vibe’, kwa hiyo hizo ni sababu zilizofanya tufanye kazi pamoja.

Mikito: Kuna tofauti gani kati ya kazi hii (Way Up) na kazi za nyuma?

Rosa Ree: Ipo tofauti kubwa, kwa sababu ngoma hii nimefanya na Emtee, zilizopita nilifanya na Bill Nas, nyingine nilifanya peke yangu na kila ngoma ina ladha yake. Lakini pia ngoma hii imeniongezea mashabiki kwa sababu Emtee ni mwanamuziki mkubwa Afrika!

 

Mikito: Umetambulisha pia menejimenti yako mpya inayokusimamia kwenye kazi zako kutoka Afrika kusini, ilikuwaje mpaka wakakusaini?

Rosa Ree: Walinitafuta na kunieleza kwamba wanavutiwa na kazi zangu na wanaomba wanisimamie. Mara ya kwanza sikuwaelewa niliona kama ni watu wanaoamua kunizingua, lakini baada ya kuzidi kunicheki tulipanga mipango mizuri ya kukutana na tukaweza kufanikisha mipango mizima ya kazi, ndiyo maana nipo nao.

 

Mikito: Utakuwa nao kwa muda gani?

Rosa Ree: Muda mrefu tu, kikubwa siwezi kuweka wazi mengi kuhusu mkataba tuliosaini.

Mikito: Baada ya kuachana na lebo yako ya kwanza ya The Industry na kufanikiwa kupata hii, umekaa muda gani bila lebo?

 

Rosa Ree: Nimekaa muda mrefu, unafika mwaka, ninamshukuru Mungu kwa hatua hii.

Mikito: Umetambulisha menejimenti sambamba na mjengo, siri ni ipi katika mjengo huo, umeununua kwa pesa ulizolipwa na menejimenti yako, pesa za muziki wako au kipi wengi hawakifahamu?

Rosa Ree: Kuhusu mjengo niweke tu wazi kwamba umenunuliwa na menejimenti yangu na wamenipa nikae kwa ajili ya kuwa ‘comfortable’ na kazi zangu. Kwa hiyo siyo mjengo wa Rosa Ree na siwezi ‘kujiachia’ eti nina mjengo kasha kushindwa kufanya mambo mengine makubwa ya kimaisha. Lakini mimi binafsi ninamiliki supermarket.

 

Mikito: Ambayo ipo wapi?

Rosa Ree: Mapinga, Bagamoyo.

Mkito: Tukizungumzia gharama, mjengo umegharimu shilingi ngapi na kwenye supermarket pia umewekeza shilingi ngapi?

 

Rosa Ree: Siwezi kuzungumzia zaidi gharama za mjengo kwa sababu siyo wangu moja kwa moja. Kuhusu supermarket ni kiasi kikubwa cha pesa, lakini sina takwimu ya mtaji moja kwa moja kwani nimeimarisha biashara hiyo taratibu, kuna muda nilikuwa nadunduliza hata siri ilimradi tu niweze kuwa na kitu changu mwenyewe.

Mikito: Kwa mwanzo huu na menejimenti yako mpya, mashabiki wako wategemee nini zaidi?

 

Rosa Ree: Mambo makubwa na kolabo za kimataifa. Nimeanza na Emtee, lakini plani ni kufanya kazi nzuri ya kunitambulisha kimataifa zaidi hata kuupeleka Muziki wa Hip Hop, Bongo huko kwenye dunia nyingine, usiishie kuwa muziki wa hapahapa tu Bongo.

Mikito: Tuna kushukuru sana Rosa Ree, mwisho kabisa video ya wimbo wako huu mpya inatoka lini?

Rosa Ree: Itatoka si muda mrefu, acha iwe ‘surprise’!

Makala: Boniphace Ngumije

WEMA Atuma Ujumbe Mzito kwa Diamond, Baada ya Nyimbo ya Iyena

Comments are closed.