The House of Favourite Newspapers

Rwanda yawataka raia mpakani kusitisha biashara na Burundi

 

SERIKALI  ya Rwanda imewataka wananchi wake walio karibu na mpaka kati ya nchi hiyo na nchi ya Burundi kusitisha biashara yoyote na majirani zao hao. Hiyo inafuatia siku chache baada ya Rwanda kuwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda.

Rwanda inazishutumu nchi hizo kwamba kusaidia makundi ya waasi yanayoipinga, anaripoti mwandishi wa  shirika la utangazaji la Uingereza (BBC),  Yves Bucyana.

 

Wito wa kuwakataza wananchi wa maeneo ya mpaka baina ya nchi hizo umetolewa na ofisa katika jeshi la Rwanda, Jenerali Mbarac Muganga, wakati wa mkutano wa usalama baina yake, wananchi na viongozi wa maeneo ya mpakani upande wa kusini-mashariki.     Jenerali Muganga amewataka kusitisha shughuli zote zinazoweza kuwalazimisha kwenda nchini Burundi hata kama itakuwa ni kuoa au kuolewa na mtu kutoka upande wa pili.

 

”Majirani wale walituchimbia shimo, kila Mnyarwanda anayekwenda huko anatupwa ndani yake, hii ni kwa mujibu wa taarifa za uhakika tulizo nazo. Hatutawashambulia nchini mwao kwani sisi tunalinda mipaka yetu. Rwanda tunajitosheleza kwa chakula ndiyo maana tunawasihi kutumia kile kidogo tulicho nacho.  Kuna wengi pia wanaokwenda kuoa au kuolewa upande wa pili wa mpakani, si kwamba tunataka kuvunja ndoa zenu lakini tunawasihi kusitisha safari za kwenda huko na vilevile kupunguza wageni mnaowapokea kutoka huko kwa sababu wanakuja wakiwa na malengo mengine mengi,” alisema Muganga .

 

Burundi imeishaitangaza Rwanda kama adui wake mkubwa.  Nchi hizo mbili zinashutumiana kuunga mkono makundi ya waasi kutoka kila upande.   Miaka mitatu iliyopita Burundi ilitangaza kusitisha biashara  na Rwanda hasa mboga na matunda na pia kusitisha misafara ya mabasi ya abiria kutoka Rwanda.

 

Rwanda imekuwa na tahadhari kubwa kwenye mipaka yake kutokana na makundi mbalimbali ya waasi yanayotishia kuishambulia.

 

Hayo yamejiri wakati ambapo Rwanda iliwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda, nchi iliyokuwa na biashara kubwa na Rwanda.   Serikali ilishutumu Uganda kwa kuwanyanyasa wananchi wake wanaokwenda ama kuishi nchini Uganda na pia kusaidia makundi ya waasi wanaotaka kuuangusha utawala wa Rais Paul Kagame.

Comments are closed.