The House of Favourite Newspapers

Sababu Za Global Publishers Kupandisha Bei Ya Magazeti

 

KAMPUNI ya Global Publishers LTD, wachapishaji wa magazeti ya Uwazi, Championi, Ijumaa, Risasi, Amani, Ijumaa Wikienda na Spoti Xtra, imepandisha bei ya magazeti yake kutoka shilingi 500 iliyodumu kwa miaka mingi hadi shilingi 800 huku Gazeti la Ijumaa likiuzwa kwa shilingi 1,000.

 

Mabadiliko hayo ya bei yameanza kutumika Juni 15, 2018 na sababu kubwa za kupanda kwa bei ya magazeti, ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, ikiwemo kupaa kwa bei za karatasi za kuchapishia magazeti na kuongezeka kwa gharama za uchapishaji.

 

Kwa kipindi kirefu, kumekuwa na uhaba mkubwa wa karatasi duniani kote na hii inatokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni sera mpya ya uhifadhi wa mazingira kupitishwa na nchi mbalimbali kupiga marufuku matumizi ya bidhaa za plastiki, ambapo uhitaji wa karatasi umepanda kwa kiwango kikubwa.

 

Sababu nyingine za uhaba wa karatasi duniani kote ni sheria za utunzaji wa mazingira ambapo ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ikiwemo utengenezaji wa karatasi, umepigwa marufuku katika nchi nyingi huku nyingine zikipunguza uvunaji wa misitu kwa kiasi kikubwa na hivyo kusababisha bidhaa hiyo kuwa adimu.

 

Aidha, sababu nyingine iliyochangia uhaba wa karatasi ni baada ya nchi ya China kuanzisha sheria mpya ya kupiga marufuku uingizaji wa karatasi zilizotumika. China walikuwa wanaingiza nchini mwao maelfu ya tani za karatasi zilizotumika, kama vile magazeti ya zamani, na kuyachakata (recycling) kwa ajili ya kutengeneza karatasi nzuri kwa matumizi mbalimbali ya uzalishaji.

 

Baada ya kuanzishwa kwa sheria mpya, China imelazimika na yenyewe kuagiza karatasi mpya kutoka nje, ambako viwanda vingi vilishasimamisha uzalishaji au kupunguza, hivyo kuongeza uhitaji (Demand) wa karatasi ili hali mgao (supply) ni mdogo.

 

Kutokana na upungufu huo wa mgao wa karatasi duniani, kulisababisha bei ya karatasi kuongezeka mara kwa mara na kuwafanya waagizaji wa karatasi nchini Tanzania nao kupandisha bei na wengine kuachana na biashara ya kuagiza karatasi kutokana na kupanda bei kila mara, hivyo kufanya upatikanaji wake kutegemea kampuni moja au mbili tu kwa nchi nzima.

 

Ndani ya kipindi cha miezi sita iliyopita, bei ya kilo moja ya karatasi ghafi imepanda zaidi ya MARA SITA. Ndani ya kipindi hicho bei ya karatasi kwa kilo moja ilianza kuuzwa kwa shilingi 1,947/= mwishoni mwa mwaka jana, ikabadilika ikawa 2,065/=, ikatoka bei hiyo hadi 2,230/=, kisha 2,419/=, 2,478/=, 2,773/= hadi 3,280/= ya sasa. Ongezeko hilo la bei ya karatasi ni karibu asilimia 70!

 

Licha ya kupanda kwa bei ya karatasi kiasi hicho, kampuni yetu iliendelea kuuza magazeti yake kwa bei ileile ya shilingi 500, isipokuwa kwa Gazeti moja tu la Ijumaa. Matarajio ya kampuni kwa kipindi chote hicho ilikuwa ni kwamba bei ya karatasi kwenye soko la dunia ingepungua na hivyo kurahisisha upatikanaji wake hapa nchini lakini hali imekuwa tofauti, karatasi zimeendelea kuadimika na bei imezidi kupanda, hali iliyosababisha kampuni kupata hasara kubwa kwa muda wote huo.

 

Imefikia mahali, viongozi wa kampuni tukatakiwa kuchagua moja kati ya mambo matatu; mosi ni kuacha kuchapisha magazeti na KUFUNGA BIASHARA kutokana na hasara tuliyokuwa tumeipata kutokana na tatizo la uhaba wa karatasi, pili KUSHUSHA UBORA wa magazeti ili kuendana na gharama za uzalishaji, au tatu KUPANDISHA BEI ili kuendelea kuwahudimia wasomaji wetu.

 

Kwetu huo ulikuwa ni mtihani mkubwa, kwa sababu kwa miaka mingi tumekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wasomaji wetu kwa kuwapasha habari kuhusu matukio ya habari za kuisadia jamii, watu maarufu, michezo na burudani kwa hiyo hatukuwa tayari siku moja msomaji wetu aamke asubuhi na kukosa gazeti kwa sababu yoyote ile.

 

Lakini pia kwa kipindi kirefu tumekuwa tukitoa magazeti yenye ubora, yaliyosheheni habari mbalimbali za kuelimisha, kuonya na kuburudisha watu wa rika zote, kuwa na gazeti bora linaloandika habari za michezo za uhakika na za kipekee, kwa hiyo uamuzi wa kupunguza ubora nao si chaguo letu.

 

Kwa hiyo uamuzi pekee tuliokuwa nao, ulikuwa ni kuongeza bei. Magazeti mengi yanayochapishwa nchini kwa sasa, ukiyatoa ya Global Publishers na baadhi ya michezo, yalishapandisha bei siku nyingi zilizopita, yakiwemo hata ya chama na serikali.

Huo ni ushahidi kwamba hata kwa magazeti ya Global Publishers, kwa hali tuliyonayo hivi sasa, kuongeza bei ni suala ambalo haliepukiki.

 

Kwa kipindi kirefu Kampuni ya Global Publishers LTD, tofauti na kampuni nyingine za uchapishaji wa magazeti, imekuwa ikitegemea mapato yake kutokana na kuuza nakala mojamoja kwa wasomaji, tofauti na wengine wanaotegemea zaidi matangazo.

 

Ieleweke kwamba uamuzi wa kupandisha bei ya magazeti, haukuwa kwa lengo la kuongeza faida bila kuzingatia hali halisi ya kimaisha ya wasomaji wetu, bali imetulazimu kufanya hivyo ili kukabiliana na gharama za uendeshaji na kuendelea kuwahudumia.

 

Tunatambua kwamba wasomaji wetu ni wa kipato cha chini na kati na kwamba tungependa kuuza magazeti yetu kwa bei wanayoimudu kama gharama za uendeshaji zingeendelea kuwa zile. Hivyo, kwa dhati kabisa, tunawaomba muendelee kutuunga mkono nasi tunawaahidi kuwa tutaendelea kuboresha magazeti yetu na kuyafanya kuwa bora zaidi na zaidi.

 

Bila wasomaji wetu kutuunga mkono, tusingefika hapa tulipo leo na siku zote, maslahi ya wasomaji wetu yamekuwa kipaumbele kwetu kwa sababu tunaamini Global Publishers ni kampuni inayomilikiwa na wasomaji, sisi tupo tu kuhakikisha tunawapa kile kitu mnachokihitaji kihabari.

 

Ni ukweli usiopingika kwamba magazeti ya Global Publishers ndiyo yanayoongoza kusomwa nchini Tanzania, yanafika hata pale mengine yanaposhindwa kufika, yanasomwa na watu wa kila rika, kutoka sehemu mbalimbali nchi nzima. Ni magazeti bora yanayopendwa na watu wengi na ndiyo maana yakaitwa Magazeti Pendwa.

 

Idadi ya nakala tunazochapisha kwa wiki, ni ushahidi kwamba tunao wasomaji wengi ambao wapo tayari kutuunga mkono katika hali zote na wanaoitakia mema kampuni yetu na ndiyo maana sisi kama kampuni pia tumekuwa mstari wa mbele kurudisha kile tunachokipata kwa jamii.

 

Tumeshaendesha promosheni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini, ambapo wasomaji wetu wawili kwa nyakati tofauti wameweza kujishindia nyumba, achilia mbali promosheni za magari, pikipiki na zawadi nyingine lukuki. Huu ni ushahidi mwingine kwamba Global Publishers ni kampuni ya wasomaji na inawajali sana wadau wake wote.

 

Licha ya ugumu huo uliotulazimu kuongeza bei kama nilivyoeleza hapo juu, kampuni inawaahidi wasomaji wote kwamba itaendelea kufanya mabadiliko makubwa katika uandishi wa habari za michezo, burudani, matukio ya wasanii, kijamii na kiuchunguzi na kampuni inawaahidi wasomaji wetu kuendelea kuwapa habari za kipekee na za uhakika.

 

Ni matumaini yetu kwamba mtaendelea kutuunga mkono, ili kuifanya Global Publishers iendelee kuongoza katika soko la habari nchini, nasi tunaahidi kuendelea kuwatumikia wasomaji wetu na Watanzania kwa jumla.

Asanteni.

E.J Shigongo

Mkurugenzi Mtendaji

Global Publishers LTD.

Comments are closed.