The House of Favourite Newspapers

Samia: Mmejenga Masoko Mbali ya Watu, Yafanyeni Kumbi za Harusi

0

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema masoko yaliyojengwa sehemu ambazo hazifikiki labda yageuzwe kumbi za harusi ili fedha zilizotumika kuyajenga zirudi.

 

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 27,2021 katika mkutano mkuu maalum wa uchaguzi viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania(ALAT) ngazi ya Taifa unaofanyika mkoani Dodoma.

 

Amesema kuna masoko mengi yamejengwa, lakini ndani matupu na anachoona ni bora halmashauri wakayageuze kuwa kumbi za harusi.

 

“Kuna masoko mengi tu, tena yamejengwa chini, yamejengwa juu. Soko la kubeba wajasiriamali 200 utakuta wapo 50 wapo 30 na huko juu hakuna watu, mkageuze tu maholi ya harusi ili yaingize fedha lakini sio maeneo ya wajasiriamali kwa sababu hakuna anayetaka kupanda juu, watu 20 utamuweka nani akae chini nani aende juu.

 

“Hapa ndipo tunaposema thamani ya fedha na ushirikishwaji wa wananchi katika kutumia fedha vile inavyopaswa, fedha nyingi mmezitumia vile isipopaswa naomba hili mkalirekebishe,”ameagiza Rais Samia.

 

Amefafanua kuwa katika ziara mbalimbali alizozifanya amebaini kutokuwepo kwa ushirikishaji wa wananchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa masoko.

 

“Tunapopita huko tunasikia malalamiko ya wananchi kuhusu masoko kwamba soko limejengwa kule sisi tupo huku, kwa hiyo sisi kutoka huko kwenda kwenye soko inakuwa ni shida.

 

“Hii ukiitazama kwa undani ni kwamba mabaraza huko ya madiwani na wengine wamekaa na kujipangia bila kuwashirikisha wawakilishi wa wananchi.

 

“Wangeshirikisha wawakilishi wa wananchi makosa ya aina hii yasingetokea, nimezunguka Dar es Salaam hapa Temeke masoko yamejengwa huko ambako hakuna watu.

 

“Sasa wanasema oooh tutajenga vivutio vya watoto ili watu wavutike kuja, tutayaweka ruti za magari ili watu wavutike kuja, lakini kabla ya ujenzi kuna kitu kinaitwa feasibility study (upembuzi yakinifu), kingefanyika vizuri soko lisingekwenda kujengwa huko.

“’Sababu haya yanavyofanyika sasa yangeonekana kama dosari na masoko yangepelekwa kunakoeleweka na kwenye wananachi,”ameeleza Rais Samia.

Leave A Reply