The House of Favourite Newspapers

Samia: Tutaendelea Kukopa, Ukisubiri Ukusanye Zako Utamaliza Kujenga Lini? – Video

0

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali itaendelea kuchukua mikopo nafuu kutoka kwa nchi wahisani, ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambao mpaka sasa gharama za ujenzi wake zimefikia shilingi trilioni 14.

 

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya tatu kipande cha Makutupora hadi Tabora, iliyofanyika ikulu jijini Dar es Salaam.

 

Ameongeza kuwa tayari ameiagiza wizara ya ujenzi na uchukuzi kukamilisha utaratibu wa manunuzi ili kumpata mkandarasi wa reli ya Tabora- Isaka na Tabora- Kigoma na baadaye Kaliua-Mpanda mpaka Kalema.

 

“Leo hii tumekusanyika hapa kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kipande cha kutoka Makutupora hadi Tabora, KM 368 na mkataba huu una thamani ya Tsh trilioni 4.41 ukijumuisha na kodi ya ongezeko la thamani.

 

“Uwekezaji mpaka sasa hivi ni Tsh tril 14.7 tusipoendelea na ujenzi wa reli tukakamilisha fedha hizi tulizozilaza chini zitakuwa hazina maana kwa njia yoyote tutakopa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo, wala kodi tunazokusanya ndani.

 

Kazi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ni kazi kubwa yenye kuhitaji uthubutu mkubwa wa Serikali na wananchi, nitumie fursa hii kuwapongeza Watanzania wote kwa mafanikio haya.

 

“Ubora wa vifaa vinavyonunuliwa uendane na reli inayojengwa kwa sababu miezi michache niliyokaa Serikali, nimeona mambo mengi sana ambayo huko nyuma yalikuwa hayafanyiki lakini sasa yanataka kufanyika, sitakubali yafanyike.

 

“Itapendeza tukimaliza kuunganisha reli humu ndani tuunganishe na nchi majirani. Tunapozubaa sisi kujenga reli, kupanua bandari, nchi zingine zinafanya hivyo. Niwaombe mnaosimamia, twendeni mimi niko nyuma, Gavana na waziri wa fedha watatuongoza kupata mikopo nafuu.

 

“Tusipoendelea na reli hii (ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza) tukakamilisha, fedha hizi tulizozilaza pale chini zitakua hazina maana.

 

“Serikali imeshangia mkataba wa ununuzi wa mabehewa ya abiria 89 vichwa vya treni ya ya umeme 19, seti za treni za kisasa 10 zenye behewa 80 na mambo yote hayo yana gharama ya jumla ya zaidi ya dola za kimarekani milioni 381.

 

“Tayari nimeshaagiza Wizara husika kukamilisha taratibu za manunuzi ili kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa kipande cha Tabora – Isaka na kipande kipya cha awamu ya pili ya ujenzi wa reli kutoka Tabora – Kigoma.

 

Uwekezaji huu ni mkubwa, tusipoendelea na ujenzi wa reli hii mpaka kukamilisha,fedha hizi tulizozitumia hazitakuwa na maana kwa hiyo, tutaangalia njia rahisi zitakazotufaa za kukopa kwa sababu fedha hizi hatutozitoa kwenye tozo wala kodi tunazokusanya ndani.

 

“Ujenzi na utekelezaji wa miradi yote iliyoanzishwa na inayoendelea tutaendelea kuisimamia, kuna wale ambao walipenda kuona miradi hii haiendelezwi na wanathubutu kusema imeshindikana, imeelezwa hapa wakandarasi hawadai hata senti moja.

 

“Ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere tunakwenda nao vizuri, hatudaiwi tunadai kazi, hakuna mradi uliosimama, mkipita barabara za Dar es Salaam kazi zinaendelea, ujenzi wa Kigongo- Busisi daraja linaendelea mabarabara huko mikoani yanaendelea.

 

“Kama walidhani kutakuwa na kusimamisha miradi wapate la kusema halipo na kuna jitihada za kutuvunja mioyo kwenye mikopo, hata nchi zilizoendelea zinakopa, kwani ukikopa unajenga haraka na mikopo hii ni ya miaka 20,kwa hiyo tutakopa na tutalipa taratibu.

 

“Ukikopa unajenga kwa haraka, ukisubiri ukusanye za kwako utamaliza lini kujenga, na wakopwaji wanakupa muda wa miaka 20, mkopo wa masharti nafuu unakudhuru nini, lakini maendeleo yanakuja haraka,” amesema Rais Samia.

 

Leave A Reply