The House of Favourite Newspapers

San; Kabila la Namibia Lililokuwa Halijui Fedha-3

0

KATIKA matoleo mawili yaliyopita nilijikita kumsimulia muigizaji maarufu X!xau aliyecheza filamu maarufu za “The Gods Must Be Crazy aliyetoka Kabila la San la Namibia.

Nimalize kwa kusema kwamba muigizaji huyu baada kumaliza maisha yake ya uigizaji huko Marekani na China aliporudi nchini kwao Namibia akiwa amestaarabika, alilima mahindi, maboga na maharage na kufuga ng’ombe kadhaa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Independent, alikuwa akijua kuhesabu moja hadi 20, hivyo hata mifugo yake ya ng’ombe walikuwa hawazidi 20 na mbuzi idadi ilikuwa hiyohiyo.

Nalo Jarida la Namibia liitwalo New Era linashabihiana na tovuti hiyo kwani nalo linabainisha kuwa muigizaji huyo hakuwa na uwezo wa kuhesabu zaidi ya 20.

Licha ya kuwa tajiri, muigizaji huyo bado hakuacha tamaduni yao ya uwindaji. Namibia anaheshimika mno kuwa ndiye msanii mkubwa na mtu maarufu zaidi kuwahi kutokea nchini mwao.

Hapo kabla hakuwa na dini kama ilivyo kwa wenyeji wengi wa kabila lake la San, hata hivyo mwaka 2000 alibatizwa na kuwa Msabato.

Bahati mbaya sana Julai Mosi, 2003, alifariki duni baada ya kuugua Kifua Kikuu lakini pia alipatwa na Nimonia, maradhi yatokanayo na baridi kali kutokana na tabia yake ya uwindaji wa ndege nyakati za usiku.

Anakadiriwa kufariki dunia akiwa na miaka 59, alizikwa kwenye makaburi ya asili huko Tsumkwe pembeni mwa kaburi la mke wake wa pili, aliacha watoto sita.

Baada ya historia hiyo sasa tuangalie mila na desturi ya Kabila la San ambalo Wazungu walikuwa wakiwaita Bushmen. Hili ni kabila ambalo linajali sana utamaduni wake.

Inasemekana limeishi katika nchi ya Namibia kwa zaidi ya miaka 30,000 kwani asili yao ni Afrika Kusini ambako wapo baadhi yao hadi sasa.

Kabila la San ni moja ya makabila ya Kiafrika kuishi kusini mwa Afrika kabla ya kuja Wazungu ambao baadaye wamekuwa walowezi.

Wanasayansi wa elimu ya viumbe na mazingira (Archaeologist) na jenetiki (Geneticists) wanaamini kwamba Kabila la San limetokana na jamii ya Homo ambayo ndiyo iliyotanda karibu nchi zote zilizopo kusini mwa Afrika na inakadiriwa kuwa jamii hiyo imeishi katika nchi hizo kwa zaidi ya miaka 150,000.

Wataalamu hao wanasema kuwa moja ya kabila la zamani sana kuishi katika ukanda huo wa Afrika ya Kusini walijiingiza katika ustaarabu miaka 80,000 iliyopita na sasa wanaitwa Khoe San.

JINA HILI LINA MAANA GANI?

Kabila hili lilipewa jina la Khoe San likiwa na maana kwamba ni Wafugaji wa San; kazi yao kubwa ni kufuga pamoja na kuwinda na unaweza kuwafananisha na Wahadzabe wa hapa Tanzania ambao ni wafugaji na wawindaji.

“Inakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 25,000 iliyopita kuwa ushahidi kwamba utamaduni wa kabila hili la San umebadilika kwa wale wanaoishi mijini tu, lakini wale wa vijijini bado wanaendeleza mila na desturi zao,” alisema mzee mmoja wa eneo hilo.

Utamaduni wa kutumia maganda ya mayai ya mbuni kutengeneza mapambo kwa wanawake wao au wasichana bado unaendelezwa hadi sasa lakini pia ile mila ya kutembea na mishale iliyo kwenye kasha maalum mgongoni na upinde kwa wanaume bado inadumishwa.

Wamekuwa wakiendelea kutembea na silaha hizo migongoni mwao na pia huko vijijini ule utamaduni wa kutovaa mashati bado na badala yake huvaa kipande cha nguo kinachofunika makalio na sehemu nyeti, utaratibu huo unadumishwa hadi leo.

Watu wa Kabila la San wanaamini sana ushirikina, wake kwa waume, wasichana kwa wavulana, ushirikina kwao ni jadi.

Je hufanya nini? Fuatilia Jumanne ijayo.

NA MWANDISHI WETU NA MITANDAO

Mbowe Kuachia Video ya Lissu Akiongea Hospitalini Kutoka Soon!

Leave A Reply