The House of Favourite Newspapers

SAYONA JUISI TAMU YA BOKSI YENYE LADHA NZURI

KAMPUNI ya Sayona Fruits Ltd, imekuja na bidhaa mpya ya juisi ya boksi na kumwaga ajira 350 za kiwandani.

 

Kampuni hiyo ambayo ni sehemu ya makampuni ya Motisun Group, katika kukuza na kutanua wigo wa uzalishaji wa bidhaa zake, imeanza kuzalisha na kufungasha juisi katika mfumo wa boksi (aseptic) kwa bidhaa mpya ya SAYONA FRUTTIS.

 

Bidhaa hii mpya inazalishwa katika ladha nne kutoka katika matunda halisi yanayochakatwa na kufungashwa katika boksi zenye ujazo wa kuanzia mililita 200, mililita 350 na lita moja. Bidhaa hizo ni za juisi za embe, nanasi, pera na mchanganyiko wa matunda yaani tropikali.

 

Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Motisun, Subhash Patel alisema maboresho hayo ya bidhaa yanaendana na sera ya Wizara ya Kilimo kuwa ustawishaji na uendelezaji wa sekta ya kilimo ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa taifa na ustawi wa uchumi wa viwanda pia.

 

“Maendeleo katika kilimo ni muhimu sana katika kutoa chakula cha kutosha na lishe bora kwa Watanzania. Hivyo sekta ya kilimo inachangia asilimia 29.1 ya pato la taifa na asilimia 65.5 ya ajira. Pia huchangia asilimia 65 ya malighafi kwa sekta ya viwanda na asilimia 30 ya pato la nje.

 

Kwa mujibu wa Patel, kampuni mpya ya Sayona Fruits Limited ambayo ipo katika Kijiji cha Mboga Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, ina uwezo mkubwa wa kuchakata, kuzalisha na kusindika katika vifungashio na ujazo mbalimbali, ikiwamo plastiki (PET) na boksi (Aseptic).

 

Alisema Kampuni ya Sayona Fruits Ltd imeanza uzalishaji na imetangaza rasmi ununuzi wa matunda kutoka kwa wakulima wadogo walio jirani na kiwanda hicho, hivyo kuwa sehemu kuu ya soko la kudumu la wakulima hao.

 

Alisisitiza pia kuwa kiwango cha ubora wa matunda hayo ni kizuri na kinakidhi vigezo. Hatua hii ya kampuni imepunguza uagizaji wa matunda kutoka nje ya nchi na kusaidia kupanua wigo kwa matunda ya ndani kukidhi viwango vya kimataifa.

 

Hadi sasa kampuni ina wakulima wapatao 122 ambao huuza mara kwa mara matunda yao aina ya embe, nanasi, pera, pasheni na nyanya. Kampuni hiyo kwa sasa ina mpango wa kuanza uzalishaji wa jams, pickles, ketchups na sauces. Ununuzi huu wa matunda utaboresha maisha na kuimarisha uhusiano na wakulima wadogo kutoka maeneo jirani.

 

KWA NINI KIWANDA KIJENGWE HAPO?

Mwenyekiti na mkurugenzi wa kiwanda hicho, Subash Patel ni mzaliwa wa maeneo ya Mboga, Msoga na Lugoba na ni maeneo ambayo baba yake alianza biashara zake nchini tangu akiwa na umri wa miaka 13.

Kiwanda hiki kitawanufaisha wazawa na kuwapatia soko la bidhaa mbalimbali za shambani. Watanzania wengi hukimbilia mjini kutafuta maisha bora ingawa hawafanikiwi.

 

Dhamira ya Patel ni kuboresha maisha ya watu wa vijijini kwa kuwasukuma kuitumia ardhi yenye rutuba katika kuzalisha mazao yatakayokuwa na thamani na tija kwa kilimo. Pia anawasaidia wakulima hao kuuza mazao yao katika maduka makubwa kwa bei nafuu na kuwawezesha kushindana katika ushindani wa soko la bidhaa za matunda.

 

Sayona Fruits Ltd imetoa ajira 350 kwa wazawa wa eneo hilo na vijiji jirani. Pia kampuni imetoa mafunzo na ujuzi mbalimbali kwa jamii husika na wafanyakazi juu ya uzalishaji wa juisi za matunda kwa kiwango cha kimataifa.

Comments are closed.