The House of Favourite Newspapers

Scorpion Aongezewa Shtaka la Kujeruhi, Arudishwa Rumande Hadi Desemba 14

scorpion-1 scorpion-2 scorpion-3 scorpion-4 scorpion-5

DAR ES SALAAM: Mtuhumiwa anayedaiwa kumtoboa macho Said Ally, Salum Njwete (34) maarufu kama Scorpion leo ameongezewa shtaka lingine la kujeruhi katika kesi yake inayoendelea kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa leo saa tatu asubuhi na Hakimu Frola Haule baada ya upelelezi kukamilika, mtuhumiwa huyo ameongezewa shitaka la pili la kujeruhi na kusomewa mashtaka yote mawili na wakili wa serikali  Nassor Katuga likiwemo lile la mwanzo la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Wakili Nassor alimsomea maelezo ya awali Scorpion yenye vipengele nane vya maswali, cha kwanza akimuuliza kama yeye ni Salum Njwete ‘Scorpion’ ambapo alikana jina hilo la Scorpion. Mtuhumiwa aliulizwa swali la pili kama anaishi Tabata Machimbo ambalo nalo alilikana.

Swali la tatu lilikuwa: “Wewe ni mwalimu wa martial art?” mtuhumiwa akakubali kuwa ndiyo ni mwalimu wa mafunzo ya kujihami bila kutumia silaha.

Wakili Nassor aliendelea na swali la nne ambapo amemuuliza kama amesomea martial art kati ya mwaka 1989 hadi 1995 huko Ifakara mkoani Morogoro ambapo pia mtuhumiwa huyo alikubali kuwa ndiyo amesomea.

Katika kipengele cha swali la tano, mtuhumiwa ameulizwa kama mnamo Septemba 6, mwaka huu alikuwa eneo la Buguruni, Sheli, ambapo Scorpion alikataa swali hilo.

Swali la sita uliulizwa kama ni kweli alimchoma visu Said Ally na kumjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili na mtuhumiwa huyo alikana kufanya hivyo.

Kisha swali la saba akaulizwa iwapo alipokuwa Buguruni, Sheli alimuibia Said Ally vitu vyenye thamani ya shilingi 331,000, jambo ambalo  mtuhumiwa pia alikana.

Katika kipengele cha mwisho, mtuhumiwa ameulizwa iwapo tarehe 12, Septemba mwaka huu alikamatwa na kukubali kuwa alimjeruhi Said Ally, Scorpion akajibu si kweli.

Baada ya maswali hayo, kesi hiyo iliahirishwa na kupangwa kusikilizwa tena Desemba 14, mwaka huu, ambapo kutakuwa na mashahidi sita, PF3 na nyaraka kutoka kwa daktari na kisha mtuhumiwa Scorpion kurudishwa rumande.

Habari / Picha: Richard Bukos na Mayasa Mariwata / GPL

halotel-strip-1-1

Comments are closed.