SERIKALI IMEANZA KUJENGA DARAJA JIPYA LA MTO WAMI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eliasi Kwandikwa.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eliasi Kwandikwa, ameliambia Bunge jana (Ijumaa) Novemba 9, 2018 kuwa mkandarasi Power Construction Corporation kutoka China amekwishasaini mkataba wa kujenga daraja jipya kwenye mto Wami, tangu Juni 28, 2018.

Kwandika ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye hakuwepo ambapo  swali hilo liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.

Mbowe ametaka kujua Daraja la Wami lilijengwa mwaka gani na kama Serikali haioni ajali zilizotokea hapo zinatokana na wembamba wa daraja na kuna mpango gani wa kupanua daraja hilo sambamba na eneo lote la barabara la mteremko wa mto huo.
“Daraja la Wami lenye urefu wa mita 88.75 lililoko mkoa wa Pwani lilijengwa mwaka 1959 na ndicho kiungo cha kutoka Chalinze kwenda ukanda wa Kaskazini,” amesema Kwandikwa.

Ameongeza kwamba daraja jipya litakuwa na urefu wa mita 513.5 na upana wa mita 11.85 na litajengwa umbali wa mita 670 pembeni mwa daraja la zamani, ambapo ujenzi utakuwa wa miezi 24 na litagharimu Sh. bil. 67.8.

Chanzo: Mwananchi


Loading...

Toa comment