The House of Favourite Newspapers

Serikali Yaipa Mtaji Kampuni Ya Mbolea Nchini(Tfc),Yaanza Usambazaji Wa Mbolea Nchini

0

Ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mbolea sahihi na bora zinawafikia wakulima wote kwa wakati na kwa bei nafuu, Serikali yaipa Mtaji wa shilingi bilioni 6 Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ili isambaze mbolea ya ruzuku nchi nzima. Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 27 Januari, 2023 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Kilimo, Mh.Anthony Mavunde alipokuwa akizindua zoezi la usambazaji wa mbolea za ruzuku za TFC.

“Ni zaidi ya miaka nane (8) sasa imepita tangu TFC mara ya mwisho wasambaze mbolea kwa wakulima. Pongezi kubwa ni kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kuwa TFC inasambaza mbolea kwa wakulima mpaka maeneo yote nchini hususani yale ambayo hayafikiwi na wafanyabiashara wengine.

Serikali inatambua umuhimu wa TFC na inafahamu kuwa mnao mtandao mkubwa na madhubuti wa usambazaji wa mbolea nchini, ni matarajio yetu mtakwenda kuutumia vizuri kufikisha mbolea hizi za ruzuku kwa wakati kwa wakulima wote nchini.


Mbolea si tu ni muhimu kwa wakulima katika kuongeza tija ya uzalishaji, bali pia ni mhimili mkubwa wa kuhakikisha nchi inazalisha zaidi na kuwa na uhakika na usalama wa chakula. Hivyo, Ninaamini kuwa, kupitia mikakati tunayoenda nayo sasa, hatutorudi tena tulipotoka miaka 8 iliyopita, na naitaka Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TFC kufanya kazi kwa uweledi na uadilifu mkubwa.

Serikali imeanza utekelezaji wa Miradi mikubwa nchi nzima ili kuwezesha Sekta ya Kilimo kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, miradi hiyo ikiwemo na ujenzi wa Mabwawa mapya 14 ya umwagiliaji ambayo yatahifadhi maji takribani lita Bilioni 131 na kuhudumia zaidi ya hekta 90,000. Ni dhahiri kwamba mahitaji ya mbolea yataongezeka ili kuendelea kuzalisha kwa tija, niwaombe TFC mchangamkie fursa hii na kufanya biashara yenye tija na faida”Alisema Mavunde

Awali, akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi,, Meneja Mkuu wa TFC Bw. Samuel Mshote aliishukuru Serikali kwa kuipa mtaji TFC na kuahidi kuwa yeye na Timu yake watasimamia ipasavyo mtaji huo ili waweze kufikia matarajio makubwa ya Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo alipongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali za kuifufua TFC na kuipa mtaji ianze kufanya biashara, na kuongeza kuwa TFRA ipo tayari kuendelea kutoa miongozo thabiti ya Udhibiti ili TFC iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), **Dkt. Florence Turuka **alishukuru jitihada za Serikali kuipa nguvu tena TFC iweze kutekeleza majukumu yake ya msingi, na kuahidi kuwa maeneo yote kwenye usambazaji wa mbolea ambayo yanakubwa na uhaba kutoka na ushindani wa kibiashara nchini, TFC ni chombo sahihi na atahakikisha kinakuwa msaada mkubwa kuondoa changamoto hizo.

Leave A Reply