The House of Favourite Newspapers

SERIKALI YAMFANYIA KITU MBAYA MO DEWJI

BILIONEA Mohamed Dewji ‘Mo’ amefanyiwa kitu mbaya na serikali baada ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula jana kutangaza uamuzi wa Serikali wa kuyafuta mashamba yake sita yenye ukubwa wa ekari 12, 915. 126 ambayo yanamilikiwa na kampuni yake ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL) yaliyopo Korogwe, Mkoa wa Tanga.  

 

Taarifa iliyotolewa kwa umma na kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo imesema uamuzi wa kufuta mashamba hayo umefikiwa baada ya mapendekezo yaliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu.

 

Imesema mapendekezo hayo yaliwasilishwa kwa Rais Dk. John Magufuli na wizara kwa nia ya kufutwa mashamba hayo ya MeTL ambayo ofisa mtendaji mkuu wake ni bilionea namba moja kijana barani Afrika, Mohammed Dewji ‘Mo.’

 

Mashamba yaliyofutwa ni yale yaliyopo eneo la Mombo, Mabogo pamoja na Kwalukonge wilayani Korogwe. Akizungumza mara baada ya kutembelea mashamba hayo, Mabula amesema yaliyobatilishwa ni kati ya mashamba 14 yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises, Mazinde wilayani Korogwe.

“Uamuzi huo unalenga kujenga nidhamu kwa waliopewa rasilimali za Serikali kuzingatia masharti ya uwekezaji, akasema mara baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kupeleka mapendekezo ya kufutwa mashamba ya Mohammed Enterprises, Wizara ya Ardhi ilifanya ufuatiliaji katika halmashauri husika kuhusu kutoendelezwa mashamba na baada ya kujiridhisha ikawasilisha maombi hayo kwa rais na kuridhiwa,” alisema Mabula.

 

Mabula amesema uamuzi huo wa rais kuridhia ubatilishaji mashamba sita kati ya 14 yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises unalenga kuhakikisha wote waliopewa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wanazingatia masharti na taratibu za uwekezaji.

Naibu waziri ameitaka halmashauri ya Korogwe kupanga mpango wa matumizi bora ya ardhi katika eneo la mashamba yaliyofutwa na kipaumbele kwa watakaopewa mashamba hayo ni wananchi waliokuwa wakiishi katika mashamba hayo na sehemu itakayobaki atafutwe mwekezaji mwingine kwa kuwa lengo la Serikali ni kuwa na uwekezaji wa viwanda.

 

Mabula amempongeza mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigella kwa kufanya kazi nzuri ya kufuatilia na kusimamia maagizo mbalimbali tangu Rais Magufuli alipoanza kubatilisha mashamba ambayo hayajaendelezwa katika Mkoa wa Tanga.

Na Mwandishi Wetu, TANGA

Comments are closed.