The House of Favourite Newspapers

Sh bil 1.3 Zamwagwa Kusajili Simba

IMEFAHAMIKA kuwa hadi hivi sasa Simba imetumia Sh Bil. 1.3 kwa ajili ya usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika huku kipa Aishi Manula na mshambuliaji wa TP Mazembe, Deo Kanda wakiongoza katika dau lao la usajili.

Timu hiyo hadi hivi sasa imewasajili wachezaji wapya tisa huku ikiwaongezea mikataba mipya nyota wake saba ambao mikataba yao imemalizika mwishoni mwa msimu uliopita. Simba imepanga kukiboresha kikosi chao kwa kusajili wachezaji bora na wenye uwezo na uzoefu mkubwa wa kucheza ligi na michuano ya kimataifa watakayoshiriki, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, timu hiyo hadi hivi sasa imetumia kiasi hicho cha fedha katika usajili wake ambao imepania kufanya vema ikiwemo kuchukua Ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Manula na Kanda ndiyo wanaoongoza katika usajili wao ambao kila mmoja amesaini kwa Sh Mil 120 huku wanafuatia kwa kuvuna dau nono ni nahodha John Bocco, Meddie Kagere, Sharaf Eldin Shiboub Ali, Clatous Chama na Erasto Nyoni waliosajili kwa Sh Mil 100 kila mmoja.

 

Wengine ni Francis Kahata, Mohammed Hussein, Ibrahim Ajibu na Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Vieira na mshambuliaji, Wilker Henrique da Silva raia wa Brazil ambao wote wamesajiliwa kwa Sh Mil 80 kila mmoja.

Anayefuatia ni beki wa pembeni, Shomari Kapombe aliyevuna Shil Mil.70, pia wapo Beno Ka
kolanya, Pascal Wawa kila mmoja alichukua Sh Mil 50 huku Kennedy Juma akisajiliwa kwa Sh Mil. 30 na kufikisha Sh bil 1.3 hadi hivi kati ya wachezaji 17 ambao tayari wamesajiliwa. “Msimu uliopita Simba tulitumia Sh Bil. 1.3 ambazo huenda zikaongezeka kwani bado tunaendelea na usajili kwa baadhi ya wachezaji wakiwemo wa ndani na nje ya nchi.

 

“Hadi hivi sasa bado hatujapiga mahesabu ya jumla ya gharama ambazo tumezitumia (lakini Championi Jumamosi tunazo) lakini tutazitangaza mara baada ya usajili wetu kukamilika,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mtendaji wa Simba, Crescentius Magori hivi karibuni aliwahi kusema kuwa: “Bado hatujajua gharama ambazo tutazitumia katika usajili wetu wa msimu ujao, lakini tumepanga kutumia zaidi ya Sh Bil 1.3 ambazo zilitumika msimu uliopita.” “Hivyo, tusubiri baada ya usajili kukamilika tutaweka gharama ambazo tumezitumia kwani bado usajili tutaendelea nao,” alisema Magori ambaye ni msomi.

Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge

Comments are closed.